MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalum Kibanda (45) amefikishwa mahakamani leo jijini Dar es Salaam.
Kibanda ambaye ni miongoni mwa wahariri nguli na maarufu nchini Tanzania amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Stewart Sanga.
Kibanda sasa anajumuishwa katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba (36) ya kuwashawishi askari na maofisa wa majeshi nchini kuacha kuitii Serikali.
Hata hivyo Mwigamba yeye hakuwepo mahakamani kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya jinai mkoani Arusha ambapo alilazimika kuhudhuria katika kesi hiyo. Kibanda katika kesi hiyo ana tetewa na mawakili wake wanne, yaani Deo Ringia, Isaya Matambo, Juvenalis Ngowi pamoja na Nyoronyo Kichele .
Akitoa maelezo mbele ya Hakimu Sanga, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda, amedai Kibanda anakabiliwa na kosa la kuwashawishi askari na maofisa wa Jeshi la Polisi, Magereza pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi nchini (JWTZ) kutoitii serikali jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 46(b), 55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Wakili huyo amedai Novemba 30, 2011, gazeti la Tanzania Daima, toleo namba. 2553 lililochini ya Kibanda (Mhariri Mtendaji), lilichapisha waraka wenye kichwa cha habari; “Waraka Maalumu kwa askari wote” ambao uliandikwa na Samson Mwigamba kupitia safu yake
ijulikanayo ‘Kalamu ya Mwigamba’.
Kibanda amekana shtaka na Hakimu Sanga kutaja masharti ya dhamana, ambayo ni mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atatakiwa asaini ‘bondi’ ya sh miloni 5 na kati yao awasilishe hati ya mali isiyoamishika yenye thamani ya fedha hiyo.
Sharti jingine ni mshtakiwa kuripoti katika kituo Kikuu cha Polisi kila mwisho wa mwezi na kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani. Mshtakiwa huyo amepata amefanikiwa kudhaminiwa baada ya kutimiza masharti yote. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 19, 2012 itakapotajwa.