Marefa wawili Tanzania waula CAF, waitwa kuwa wakufunzi

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

WATANZANIA Leslie Liunda na Joan Minja wamechaguliwa kuwa wakufunzi wa waamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) baada ya kufaulu katika kozi iliyofanyika Mei mwaka jana jijini Cairo, Misri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Dar es Salaam na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na Ofisa Habari wake, Boniface Wambura imesema kuwa.

Taarifa hiyo imesema Minja pia ni Katibu wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Liunda ni miongoni mwa zaidi ya waamuzi wa zamani 90 walioshiriki kozi hiyo ambapo jumla ya waliofaulu na kupata ukufunzi wa CAF ni 58 wakiwemo wanawake tisa.

Ukanda wa CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati) umetoa jumla ya wakufunzi tisa kutokana na kozi hiyo. Wakufunzi hao kwa upande wa wanawake ni Minja (Tanzania), Gladys Waweru (Kenya) na Catherine Adipo (Uganda).

Kwa upande wa wanaume ni Liunda (Tanzania), Ali Waiswa (Uganda), Bernard Mfubusa (Burundi), Eshetu Sheferaw (Ethiopia), Jumaa Kaluwe (Kenya) na Salih Mohamed (Sudan). Watanzania wengine ambao waliwahi kuwa wakufunzi wa waamuzi wa CAF ni Gratian Matovu, Joseph Mapunda na Alfred Lwiza.