Na Mwandishi Wetu
MABONDIA Rashid Matumla ‘Snake Man’ na Maneno Oswald ‘Mtambo wa Gongo’ wanatarajia kupanda ulingoni Desemba 25 mwaka huu katika pambano lisilo la ubingwa, wamepima uzito na kukutwa wapo fiti kiafya.
Pambano hilo la raundi 10 uzito wa kati litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Heinken, Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam.
Daktari wa mchezo wa ngumi nchini, Charles Kilaga, aliyewapima na kukuta wapo fiti alisema sheria za mchezo huo azirusu mchezaji kutumia dawa za aina yoyote ya kuongeza nguvu mwilini kwake.
Mabondia Rashidi Matumla na Maneno Oswald walikubaliana kupima uzito na vipimo mbalimbali vikiwemo vya Ukimwi siku 10 kabla ya mpambano wao utakaopigwa Jumapili ya Desemba 25, 2011.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Adios Promotion, Shabani Adios ‘mwayamwaya’ ambaye ndiye muandaaji wa pambano hilo, alisema pambano hilo limeandaliwa ili kumaliza ubishi baina ya mabondia hao, ambapo katika pambano lao la mwisho Matumla alimchapa Oswald kwa pointi.
Hata hivyo, Oswald aliwalalamikia majaji kuwa hawakumtendea haki. Katika historia ya mapambano yao ya nyuma, Matumla alimshinda Maneno Mara mbili na Maneno kushinda mara moja.
Mpambano huo utasindikizwa na mabondia mkongwe Rashidi Ally atazichapa na Kulwa Mbuchi, Selemani Jumanne na Ibrahimu Madeusi wakati Shabani Zunga atavaana na Mohamedi Kashinde, na bondia Sweet Kalulu na Saleh Mtalekwa.
Katika Mchezo huo kutakua na ‘DVD’ za mafunzo ya mchezo wa ngumi pamoja na kutambua sheria zake mbalimbali zitakazokua zikisambazwa na kocha wa mchezo huo Rajabu Mhamila ‘Super D Boxing Coach’ kwa ajili ya kuwapa mambondia mbalimbali mbinu za mchezo na mashabiki kujua sheria za masumbwi.
“Kuna mapambano kama ya akina Amir Khan, Manny Paquaio, Floyd Maywhether, David Haye, Mohamedi Ali pamoja na mtanzania Roja mtagwa anaefanya shughuli zake Marekani,”
Chanzo; Super ‘D’ Boxing Coach