Usiyoyafahamu kuhusu Mchungaji Mwasapila

 

Mch. Ambilikile Mwasapila

HIVI unafahamu kwamba Mchungaji Ambilikile Mwasapila ambaye umaarufu wake umepanda kwa kasi kutokana na kutoa tiba ya magonjwa sugu, ni yatima ambaye hakuwahi kuwafahamu baba na mama yake?

Mwasapila ambaye ni Mchungaji Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), anasema hakuwahi kuwatambua wazazi wake kwani walifariki dunia akiwa na umri mdogo hivyo kulelewa na wajomba zake.

“Niliambiwa kuwa baba yangu alifariki nikiwa mchanga na baadaye mama yangu kufariki nilipokuwa nikianza kutembea, hivyo sikuweza kuwatambua,” anasema Mchungaji huyo alipozungumza na Mwananchi nyumbani kwake, kijijini Samunge, Loliondo huko Arusha.

Hata hivyo, Mchungaji huyo anaonekana kutopenda kuingia kwa undani katika masuala yanayohusu historia yake na familia anakotoka kwani hata alipoulizwa majina ya wazazi wake hao alisema kwa ufupi tu kwamba “…sidhani kama majina yao yana umuhimu.”

Pia hakuwa tayari kuzungumzia habari za ndugu zake wengine lakini aliweka wazi kwamba kwa mama yake yeye ni mtoto wa pekee, wa mwanzo na mwisho yaani ‘Alfa na Omega’. Hii inamaanisha kwamba ndugu zake wengine ni watoto wa baba yake.

Haiba yake

Kama sura yake ya upole inavyoonekana kwenye taswira ya picha, ndivyo Mchungaji huyo alivyo. Ni mpole na mtulivu hasa anapokuwa katika mazungumzo na mtu yeyote.

Anaonekana kuwa mtu asiye na haraka hata kidogo katika utendaji wa mambo yake. Ukimtazama kwa haraka unaweza kuwa na hitimisho lisilo sahihi kwa kumdhania kuwa pengine ni mtu asiyejali.

Unapomuuliza swali anatulia kwanza kama sekunde tano hadi kumi hivi kabla ya kutoa majibu, taratibu. Mara zote hana majibu marefu, ni mafupi lakini yanayojitosheleza.

Tabia hii ya Mchungaji Mwasapila ni miongoni mwa mambo yanayomjengea umaarufu mkubwa, kwani pale anaposimama na kuinua kinywa chake kusema neno lolote mbele ya umati wa watu wanaofika kunywa dawa, basi umati huo hutulia na kumsikiliza kwa umakini mkubwa.

Kama haiba yake ilivyo, ndivyo maneno yake pia yalivyo. Mara zote anapokuwa akizungumzia maisha na huduma yake, hutanguliza neno Mungu, akimaanisha kwamba Mungu ndiye anayestahili kupewa utukufu katika kila jambo.

Kuzaliwa na maisha yake

Mchungaji Mwasapila alizaliwa katika Kijiji cha Ibililo kilichopo Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya mwaka 1936, ikimaanisha kwamba ana umri wa miaka 75 hivi sasa.

Anasema katika kukua kwake alipitia katika mchakato wa ngazi mbalimbali za elimu ambazo hata hivyo, hakuziweka wazi kutokana na ufinyu wa muda, lakini anabainisha kwamba elimu yake ilimwezesha kuwa fundi mwashi, akijenga majengo mbalimbali.

Mwaka 1963, akiwa na umri wa miaka 27 alihamia Babati, mkoani Manyara ambako ndiko alikoweka makazi yake ya kudumu hadi alipoitwa na Mungu kumtumikia mwaka 1968.

“Nilihamia Babati mwaka 1963 na hapo ndipo nilipoweka makao yangu hadi sasa, ijapokuwa katika wito wa huduma hii nalazimika kukaa hapa Samunge nikiwahudumia wahitaji kama Mungu alivyonituma,” anasema Mchungaji huyo kwa sauti ya upole.

Anasema katika kutafuta maisha, amepotezana na ndugu zake siku nyingi: “Ninaamini ndugu zangu wapo huko Mbeya pengine na kwingineko lakini sijawasiliana nao siku nyingi sana… kweli ni siku nyingi, sina mawasiliano nao.”

Jina na familia yake

Tangu alipoanza kutoa tiba, Mchungaji huyu amekuwa akitajwa kwa majina yanayotofautina. Vyombo vya habari vinamtaja kwa majina tofauti na yeye hilo anasema halimsubui hata kidogo. Jina lake la kwanza limekuwa likitajwa kuwa ni Ambikile na wengine kutaja kuwa ni Ambilikile.

“Wanataja kama wanavyotaja mimi hainipi shida, ila ukitaka kunyoosha vizuri (kutamka kwa usahihi) mimi naitwa Ambilikile Mwasapila, maana ya jina Ambilikile ni “ameniita”, yaani Mungu ameniita.” Vyombo vya habari vimekuwa vikitaja jina lake la pili kuwa ni Masapila, Mwaisapila na Mwasapile.

Kuhusu familia anasema alibahatika kuoa, lakini Mungu alimwita mke wake mwaka 2009. Anasema ni imani yake kwamba Mungu alipenda kumwita mkewe hivyo hana hoja juu ya kifo chake.

Anasema katika maisha yake ya ndoa, Mungu aliwajalia kupata watoto sita, wawili ni wa kike na wanne wa kiume… “Wengine wako katika maeneo mbalimbali nchini ila mmoja wa kiume niko naye hapa Samunge.”

Tiba ya magonjwa sugu

Mchungaji Mwasapila anasema alipata ndoto kutoka kwa Mungu kuhusu utoaji wa tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi kwa mara ya kwanza Januari 10, 1991 na ndoto hiyo kujirudia Oktoba 9, 2006.

Anasema kutokana na ndoto hizo, aliendelea kusubiri maelekezo ya Mungu na kwamba ilipofika mwaka 2009 ndoto hizo ziliendelea kumjia mfululizo. Hivyo kuanza kutoa tiba hiyo baada ya kuwa amepata kile anachokiita ‘tangazo la Mungu.’

Miongoni mwa hatua ambazo alizipitia kabla ya kuanza kutoa tia hiyo ni kuutambua mti wa mugariga, utaratibu wa kutoa tiba hiyo, kipimo cha dawa wanachopaswa kupewa wagonjwa, jinsi ya kuwapata wagonjwa husika na gharama kwa dawa kwa wagonjwa.

Kikombe cha babu

Dawa yote wanayokunywa wagonjwa wanaofika katika Kijiji cha Samunge lazima ipitie katika mkono wa Mchungaji Mwasapila.

Mkono wa mtumishi huyu wa Mungu huwa umeshikilia kikombe maarufu kama “kikombe cha babu”, ambacho hukitumia kuchota dawa kutoka kwenye ndoo ambazo huletwa na wahudumu. Anachiokifanya ni kujaza vikombe vingine ambavyo hutumiwa na watu kunywa dawa hiyo.

Wakati wote utamwona Mchungaji Mwasapila akiwa na kikombe hiki mkononi mwake, huwa hakiachi popote anapokwenda labda kama si wakati wa kutoa dawa. Hapa ina maana kwamba hata kama akienda kupata chakula cha mchana au chai ya saa nne, babu huondoka na kikombe chake.

Wakati akieleza kuhusu kikombe hiki, Mchungaji Mwasapila alikuwa na uso wa tabasamu kwa mbali, hii inaashiria kwamba kikombe chake kina thamani kubwa katika utoaji wa dawa au tiba kwa wengine tunavyoweza kutamka.

Anasema kwa kuzingatia kazi zake za ufundi uashi, wakati fulani alilazimika kuwepo Mjini Loliondo ambako alikuwa akijenga nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki.

Anasema baada ya kukamilisha ujenzi huo uliochukua siku kadhaa, alirejea nyumbani kwake, Samunge ambako alikuta kikombe ndani ya nyumba yake kikiwa kikizagaa.

“Niliwauliza wale vijana niliowaacha pale nyumbani… Jamani hiki kikombe ni cha nani? lakini kila mmoja alisema hajui na wala hawakufahamu jinsi kilivyoingia ndani ya nyumba yangu.”

Anasema walijaribu kuwauliza hata majirani iwapo kuna mtu ambaye kwa namna moja au nyingine alikuwa amesahau kikombe kile, lakini hakuna aliyejitokeza hivyo kukiacha ndani bila matumizi na kwamba kilikuwa kipo kipo tu ndani ya nyumba hiyo.

Kwa mujibu wa Mwasapila, baada ya muda mrefu kupita (hakumbuki ni muda gani), alilazimika kumuuliza Mungu kipimo cha dawa aliyoonyeshwa kuitoa kwa watu na hapo ndipo alipoonyeshwa kikombe hicho ambacho anasema wakati wote kilikuwa kikizagaa ndani ya nyumba yake.

“Mara moja nilinyanyuka nikaenda kukichukua kikombe, na hapa ndipo nilipojua thamani yake, Mungu alisema kikombe ndicho kipimo sahihi na mtu anatakiwa kunywa kimoja tu na watoto ni nusu yake”, anasema.

Baadhi ya Vigogo wa Serikali, Dk. Yohana Balelel na Abas Kandoro, ambao ni wakuu wa Mikoa wakipata Kikombe kwa 'Babu'

Neville Meena na Mussa Juma, Samunge (Mwananchi)