Mahakama Kuu Tanzania yasajili mawakili 315 wapya

Jaji Mkuu wa Tanzania, Chande Othuman.

Na Mwandishi wetu

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imewasajili na kuwatambua mawakili wapya 315. Zoezi hilo la usajili limefanyika jana jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu Chande amesema bado sekta ya Mahakama inakabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji wa mashauri mbalimbali yanayowasilishwa pamoja na ukosefu wa uelewa wa sheria miongoni mwa wananchi hasa wa mikoani.

Jaji Chande amesema wananchi wengi hasa wanaoishi vijijini wamekuwa wakishindwa kupata haki zao za msingi kutokana na uelewa mdogo wa sheria ikiwa ni pamoja na kukosa huduma za mawakili kutokana na uchache wa kundi hilo muhimu.

Ameeleza kuwa mawakili waliosajiliwa watafanya kazi za kisheria katika sehemu tofauti ikiwa ni pamoja na kwenye sekta binafsi, kampuni, idara, halmashauri na kwenye vyuo mbalimbali vilivyopo ndani na nje ya nchi hivyo amewataka kufuata taratibu na kanuni za kiwakili.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Warema akizungumza kwenye hafla hiyo ametoa wito kwa mawakili kujitokeza na kutoa michango katika mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya kwani suala hilo linategemea zaidi masuala ya kisheria.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Jaji Fransis Stolla amewataka mawakili waliosajiliwa kuzingatia kuwa kulinda na kutetea umma ndiyo wajibu wao mkuu hasa pale umma unapohitaji msaada wa kisheria.

Amewataka mawakili hao pindi wanapokuwa katika shughuli zao kufanya kwa uadilifu mkubwa ili kuonesha kuwa ni watu bora na wenye sifa stahili kutokana na baadhi yao wanapopata nyadhifa hizo kujiingiza katika vitendo vya upokeaji rushwa na kutotenda haki. Tanzania ina jumla ya mawakili 2,500 ambao hawatoshelezi kutokana na idadi ya watanzania ambao kwa sasa wanafikia zaidi ya milioni 44.