Waziri Mkuu Tanzania ahimiza uwekezaji kikanda Kilimanjaro

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Mkoa wa Kilimanjaro (KDF) na Waziri Mkuu Mstaafu,Cleopa Msuya (wapili kushoto) na Makamu wake, Anald Kileo (kushoto baada ya kufungua mkutano wa KDF kwenye hoteli ya Kilimanjaro Cranes Mjini Moshi, Desemba 15,2011. Wapili kushoto ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Mbunge wa Siha, Aggrey Mwanri. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na Mwandishi Maalumu, Kilimanjaro

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amesema Mkoa wa Kilimanjaro unaweza kuwa kitovu cha maendeleo katika kanda ya Kaskazini kama ukijipanga vizuri na kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa huo.

Ametoa kauli hiyo leo mchana Desemba 15, 2011 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Kilimanjaro (Kilimanjaro Development Forum – KDF) unaofanyika katika hoteli ya Cranes, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amezitaja fursa hizo kuwa ni utalii mkubwa uliopo kwenye mkoa huo, umeme, uwanja wa ndege, barabara za lami za km 443, huduma za jamii za muda mrefu, idadi kubwa ya wasomi na tabia ya ujasiriamali ya wakazi wa mkoa huo.

Amesema Mkoa wa Kilimanjaro uangalie fursa iliyonayo ya kujiunga na mikoa jirani ya Tanga, Arusha na Manyara na kusukuma jitihada za maendeleo kwa pamoja badala kutaka kwenda mbele yake.

Waziri Mkuu amesema anatambua changamoto ya uhaba wa ardhi inayoukabili mkoa huo lakini akatumia jukwaa hilo kuwasihi wakazi wa mkoa huo waangalie fursa ya kuwekeza katika mikoa mingine yenye ardhi kubwa na waache tabia ya kung’ang’ania robo ekari walizoachiwa na babu zao.

“Nawasihi pia muangalie fursa za kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na siyo kwa kilimo peke yake…mnaweza kutenga maeneo kwa ajili ya EPZ au SEZ na watu wakaja kujenga viwanda ambavyo vitasadia kutoa ajira kwa ajili ya vijana wa mkoa wenu,” alisema.

Alilitaka Jukwaa hilo (KDF) lishirikiane na uongozi wa mkoa huo kwa kutoa ushauri katika masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mkoa huo.

Mapema akitoa taarifa kuhusu KDF, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya alisema jukwaa hili lilifanya utafiti kuhusu kilimo cha zao la vanilla katika mkoa huo ili kuwa na zao mbadala la kahawa ambalo limekuwepo mkoani humo kwa muda mrefu lakini hivi sasa uzalishaji wake umeshuka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema mkoa unakabiliwa na changamoto ya kukua kwa kasi ili kukabiliana na hadhi za majiji jirani ya Nairobi, Mombasa, Arusha na Tanga.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, mkoa wake umeazimia kwamba ajenda ya uwekezaji iwe ndiyo kipaumbele kikubwa katika vikao vyote kuanzia ngazi za wilaya hadi mkoani.