Rais Kikwete aenda Uganda kuhudhuria mkutano wa ICGLR

Pichani kushoto anayepunga mkono ni Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete mara alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. (Picha na Ikulu)

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameondoka nchini leo, Desemba 15, 2011, kwenda Kampala, Uganda ambako ataungana na viongozi wenzake wa nchi za Maziwa Makuu kuhudhuria Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu wa International Conference on the Great Lakes Region (ICGLR).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kuufikia mtandao huu kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ni kwamba, mkutano huo utakuwa wa siku mbili, ambapo licha ya kujadili mambo mengine, utakuwa na kikao maalum cha kujadili Ukatili wa Kinjisia (Sexual Gender Based Violence)- kama ilivyoamuliwa katika mkutano wa mwaka jana uliofanyika Lusaka, Zambia.

Kikao hicho cha Kampala pia kitawapa nafasi wakuu hao wa nchi kujadili na kuangalia upya ripoti ya Mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi na Usalama wa eneo la ICGLR kuhusiana na majeshi hasi yanayoendelea kusumbua na kuyumbisha eneo hilo la Maziwa Makuu.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa ICGLR, Balozi Liberata Mulamula, wakuu hao wa nchi pia watapata nafasi ya kujadili na kuamua kuhusu ombi la taifa jipya la Sudan Kusini kujiunga na ICGLR.

Aidha, Rais Kikwete na wakuu wenzake wa nchi wanachama wa ICGLR pia watapokea ripoti ya maendeleo ya utekelezaji kuhusu maamuzi yaliyofanyika katika kikao cha mwaka jana mjini Lusaka na hasa kuhusu Jitihada za Nchi Wanachama wa ICGLR Kupambana na Uvunaji na Biashara Haramu ya Maliasili ya nchi wanachama.

Kikao cha Kampala pia kitateua Katibu Mtendaji mpya wa ICGLR kuchukua nafasi ya Balozi Mulamula wa Tanzania ambaye aliongezewa muda wa mwaka mmoja katika kikao cha mwaka jana ili kutoa nafasi kwa nchi wanachama kuwasilisha majina ya wanaofaa kuwania nafasi hiyo.

Mpaka sasa wagombea watatu wamejitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Profesa Lumu Alphonse Ntumba Luaba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Balozi Philip Richard Okanda Owade wa Kenya na Dk. Mohammed Abdleghaffar wa Sudan.