Kambi ya Ngumi Ilala kumuandaa bondia Ubwa Salum

KAMBI ya Mchezo wa Ngumi ya Mkoa wa Kimichezo wa Ilala, Dar es Salaam, inamuandaa bondia Ubwa Salum kwa ajili ya pambano lake dhidi ya bondia Mustafa Dotto, litakalofanyika Desemba 25 mwaka huu.

Akizungumza jana Dar es Salaam Kocha Msaidizi wa Kambi Ilala, Rajabu Mhamila ‘Super D’ alisema pambano hilo litakuwa kati ya mapambano yatakayotangulia katika pambano kali linalowakutanisha mabondia Maneno Osward pamoja na Rashid Matumla (la raundi 10), litakalochezwa Siku ya Sikukuu ya X-Mass.

“Tunamuandaa bondia wetu ili aweze kujiweka vizuri na pambano lake, hivyo tunatarajia kuwa atafanya vizuri kutokana na maandalizi,” alisema.
Aidha aliongeza kuwa pambano hilo la utangulizi litakuwa la uzito wa Light lenye raundi sita litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Heinken Mtoni Kijichi.

Akizungumzia pambano kuu, Super ‘D’ alisema kuwa mabondia hao wameshawahi kukutana mara tatu mpaka sasa ambapo Matumla alishinda mara mbili na Osward alishinda mara moja, jambo ambalo linaashiria mpambano kuwa mkali.

“Pambano kati ya Osward na Matumla linatarajiwa kuwa la aina yake kutokana na kuwa mabondia wote ni wazuri na wana uwezo mkubwa ulingoni” alisema

Mbali na kuwepo mapambano ya ngumi kutakuwa na uuzwaji wa DVD zenye mapambano ya mabingwa wa Dunia akiwemo Manny Paquaio, Floyd Maywherth, Roy Jones na wengine kibao ‘DVD’ hizo zilizoandaliwa kwa ubora wa hali ya juu zitakuwa zikiuzwa kwenye mpambano huo na Kocha Rajabu Mhamila ‘Super ‘D’.

“Ninatarajia kuwapelekea DVD mashabiki wa ngumi watakaokuwepo katika pambano la Cheka na Maugo ili kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sheria za mchezo wa ngumi,” alisema Super ‘D’

Chanzo: Super D Boxing Coach