MAREKANI imesema uchaguzi uliofanyika hivi karibuni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ulikuwa na dosari nyingi, hivyo kutaka mchakato wa tathmini urejewe upya.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yamempa, Rais Joseph Kabila ushindi wa asilimia 49 dhidi ya asilimia 32 alizojipatia kiongozi wa upinzani na mpinzani mkuu wa Kabila, Etienne Tshisekedi.
Taarifa kutoka Marekani zinasema, hata hivyo matokeo hayo yamekosolewa na Jumuiya ya Ulaya, kituo cha Carter Center na waangalizi wengine wa uchaguzi. Balozi wa Marekani nchini humo anasema kumekuwa na “dosari kadhaa”.
“Marekani inaamini kuwa uendeshwaji wa uchaguzi huu ulikuwa na dosari,” Balozi James Entwistle alisema katika taarifa kwa Shirika la Habari la Reuters. “Uchaguzi haukuwa wazi na haukuzingatia mafanikio ya demokrasia yaliyoonekana katika chaguzi za nchi zingine barani Afrika,” alisema.
Entwistle alisema Marekani na wafadhili wengine kutoka nchi za Magharibi wanatoa msaada wa kiufundi kwa Congo ili kuchunguza kwa makini dosari zilizotambuliwa na waangalizi wa uchaguzi, jambo ambalo tayari limeafikiwa na waziri mkuu wa nchi hiyo, alisema.
-BBC