Serikali kusitisha uuzaji wanyamapori hai

Mnyamapori hai

Na Bebi Kapenya – MAELEZO

SERIKALI imepiga marufuku ukamataji, uingizaji na usafirishaji wa wanyamapori hai isipokuwa kwa wadudu, ikiwa ni amri ya katazo juu ya vitendo hivyo yaani ‘The Wildlife Conservation’ (Capture of Animals) (Prohibition) Order, 2011.

Tamko hilo limewekwa hadharani jana na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, George Matiko, ikiwa ni kutokana na tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 435 la Desemba 9, 2011.

Hata hivyo, wafanyabiashara wenye vibali halali vya kumiliki na kusafirisha wanyamapori hai ambavyo hadi Agosti 18, 2011 vilikuwa havijamaliza muda wake kisheria wanatakiwa kusafirisha wanyama hao ndani ya siku 90 tangu Desemba 9, 2011.

Tangazo hilo la Serikali limetolewa na kutambua kuwa wakati amri ya kusitisha biashara ya wanyamapori hai ilipotolewa Julai 18, 2011, kuna baadhi ya kampuni ambazo tayari zilikuwa na wanyamapori katika mazizi yao waliokuwa wamekamatwa kwa mujibu wa sheria.

Muda uliotolewa kwa wafanyabiashara ni kwa mujibu wa Kanuni za Ukamataji wa Wanyamapori za mwaka 2010 zilizotangazwa kwa Tangazo la Serikali Na. 244 la Julai 2, 2010. Kanuni ya 12(4) na (5) ya kanuni hizo inaelekeza kuwa wanyamapori waliokamatwa kwaajili ya usafirishaji nje ya nchi kibiashara wanatakiwa wawe wamesafirishwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu kukamatwa.

Vilevile, kutokana na Tangazo hilo (Na. 435 la Desemba 9, 2011) Wizara imezuia ukamataji, uingizaji na usafirishaji wa wanyamapori hai isipokuwa wadudu tu (Class 21).

Serikali kupitia Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa matumizi mengine ya wanyamapori hai pamoja na mazao yake kwa shughuli zisizo za kibiashara na zenye manufaa kwa Taifa, kama vile utafitii, yanaruhusiwa.