Rais Kikwete afanya mazungumzo na Benki ya AfDB

Rais Kikwete akiwa na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Bi. Tonia Kandiero aliyemtembelea leo Jumanne Desemba 13, 2011 na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam. (PICHA NA IKULU)

Na Mwandishi Maalumu

RAIS Jakaya Kikwete leo katika Ikulu ya Dar es Salaam amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi kazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Dk. Tonia Kandiero.

Dk. Kandiero amefika Ikulu kujitambulisha baada ya kuanza kazi hapa nchini mwezi Mei, mwaka huu kuchukua nafasi ya Dk. Sipho Moyo ambaye alimaliza muda wake hapa Tanzania.

ADB ni moja ya wahisani wakubwa hapa Tanzania ambapo sehemu kubwa ya misaada yake inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na hasa sekta za barabara, Kilimo, Maji na Nishati.

Dk. Kandiero pia amefika Ikulu kumueleza rasmi Rais Kikwete kuhusu mkutano mkuu wa magavana wa benki hiyo utakaofanyika mjini Arusha tarehe 30 Mei – 01 Juni, 2012.

Mapema kabla ya kuonana na mwakilishi wa AFDB, Rais Kikwete amekutana na Balozi Sander Gurbuz wa Uturuki ambaye amefika Ikulu kumuaga Rais Kikwete baada ya kufikia ukingoni mwa muda wake wa kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania.

Nchi ya Uturuki imefungua ubalozi wake kwa mara ya kwanza hapa Tanzania mwaka 2009 na Balozi Gurbuz ndiye amekua muanzilishi wa Ubalozi huo.

Tangu kufunguliwa kwa Ubalozi huo, mahusiano baina ya Uturuki na Tanzania yamekua kwa kiwango kikubwa na miradi mbalimbali ya maendeleo, kibiashara na kijamii imeanza na kuimarika katika kipindi chake.

Miradi hiyo ni pamoja na kuanza kwa safari za ndege kati ya Tanzania na Uturuki, miradi ya shule na fursa za mbalimbali za masomo na biashara baina ya wananchi wa nchi hizi mbili.