Mechi za Tusker Chalenji zaingiza mil 267

Moja ya michezo ya CECAFA Tusker Chalenji katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu

MECHI 26 za michuano ya 35 ya CECAFA Tusker Challenge Cup iliyofanyika Dar es Salaam kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 mwaka huu, zimeingiza jumla ya sh. 267,066,000. Michuano hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ilishirikisha timu za mataifa 12.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na TFF, inasema katika hatua ya makundi ya michuano hiyo iliingiza sh. 145,613,000, robo fainali (sh. 58,470,000), nusu fainali (sh. 55,787,000) wakati fainali iliingiza sh. 17,196,000. Kila siku zilichezwa mechi mbili isipokuwa Novemba 26 mwaka huu ambapo ilikuwa siku rasmi ya ufunguzi na Novemba 28 mwaka huu zilichezwa mechi tatu.

Taarifa hiyo ilisema mechi iliyoingiza fedha nyingi kuliko zote ilikuwa ya ufunguzi hatua ya makundi kati ya Tanzania na Rwanda ambapo zilipatikana sh. 64,178,000 wakati fedha kidogo (sh. 446,000) zilipatikana kwenye mechi kati ya Uganda na Somalia iliyochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Azam.

Jumla ya washabiki walioshuhudia michuano hiyo walikuwa 103,312. Washabiki walioshuhudia hatua ya makundi walikuwa 65,617, robo fainali (17,844), nusu fainali (16,014) wakati fainali walikuwa 4,837.

“Mechi iliyokuwa na washabiki wengi zaidi ni kati ya Tanzania na Rwanda ambapo waliingia 23,946 wakati iliyoingiza wachache ni 446 walioshuhudia mechi kati ya Somalia na Uganda,” ilisema taarifa hiyo.

“Tunawashukuru wadhamini wakuu Tusker na washabiki waliojitokeza kushuhudia michuano hiyo. Vilevile Kampuni ya mafuta ya Gapco, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na PSPF, na pia wadau wengine waliofanikisha mashindano hayo kwa njia mbalimbali akiwemo Zacharia Hanspope,” ilieleza taarifa hiyo.