RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila amekanusha vikali madai ya kwamba alishinda uchaguzi wa nchi hiyo kupitia wizi wa kura.
Waangalizi kutoka wakfu wa Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter walisema matokeo ya uchaguzi huo hayakuwa ya kuaminika, na pia Askofu wa mkuu wa kanisa Katoliki mjini Kinshasa akasema matokeo hayo hayakudhihirisha ukweli halisi.
Taarifa zaidi zinasema Kabila, licha ya kukanusha madai hayo amekiri kuwa kulikuwa na dosari kadhaa katika uchaguzi huo. Kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi alidai ndiye aliyeshinda. Watu wasiopungua wanne waliuwawa kwenye maandamano mwishoni mwa wiki ya kupinga matokeo rasmi yaliyompa Rais Kabila ushindi wa asilimia 49 dhidi ya asilimia 32 aliyopata mgombea Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 78.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Kabila mwenye umri wa miaka 40 amepuuzilia mbali madai kwamba matokeo hayo hayakuwa halali. “Hakuna shaka yoyote, matokeo haya ni halali,” Kabila aliambia waandishi.
Alitaja kwamba kura chache alizopata kwenye mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ni dhihirisho kwamba mchakato wa uchaguzi ulikuwa wazi. Amesema hajashangazwa na hatua ya Tshisekedi kujitangaza yeye ndiye Rais, lakini akasema ataendelea na kazi yake ya kuiongoza Congo, na kwamba ana imani kuwa uchumi wa nchi hiyo utakuwa kwa kiasi kikubwa katika miaka miwili au mitatu ijayo.
Vyama vya upinzani vimetangaza mipango ya kufanya maandamano baada ya kukataa ushindi wa Kabila. Wagombea wengine wanne kwenye uchaguzi huo wamesema lazima urudiwe wakisema kulikuwa na wizi wa kura.
-BBC