*Nape apinga wazo la wabunge kujipandishia posho
Na Joachim Mushi
KUNA dalilizote kuwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hauridhiki na baadhi ya vitendo na uamuzi unaofanywa na wabunge wa chama hicho ndani ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania.
Tayari jana uongozi wa Chama Cha Mapinduzi, kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye umetoa taarifa ya kuwapinga wabunge hao ambao wanakamilisha taratibu za kujipandishia posho za vikao vya siku kutoka 70,000 hadi 200,000 kwa siku.
Spika wa Bunge Anne Makinda hivi karibuni alizungumza na vyombo vya habari akitetea hoja ya ombi lao ambalo tayari wameliwasilisha kwa Rais Kikwete wakitaka wapandishiwe posho hizo, ilhali hali ya Watanzania wengi kwa sasa kimaisha ni duni.
Hata hivyo CCM ambayo ndiyo yenye wabunge wengi Bungeni wamekuwa wakionesha nia ya kujiongezea posho za wabunge, huku msimamo huo ukipingwa na wabunge wengine hasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika taarifa ya CCM jana imesema wamefuatilia kwa makini suala hilo la nyongeza ya posho kwa wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila na Spika wa Bunge Anne Makinda- nakuona si vema nyongeza ya posho ifanyike.
“…Kwa namna suala lenyewe linavyopewa msukumo, CCM imeona si vema kukaa kimya na hivyo imetoa msimamo wake kama ifuatavyo; linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu wa maisha au kupanda kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache ndani ya jamii.
“Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza pengo/tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi,” imesema taarifa hiyo ya Nnauye.
Amesema, Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kwamba sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma kama alivyoainisha Spika wa Bunge, ndiyo inasababishahofu na mashaka miongoni mwa Watanzania.
“Na kwa kweli swali kubwa kwa Watanzania hao ni je, maisha yanapanda Dodoma pekeake na kwa wabunge tu? Hivyo basi CCM inashauri kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi na jamii yetu kwa ujumla, waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na swala hili, kulitafakari upya jambo hili,” amesema Nnauye katika maelezo yake.
Aidha ameongeza kuwa CCM inaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo Walimu, askari, Madaktari na wengineo.
Ameongeza kuwa ni vema ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.
Hata hivyo, katika hatua nyingine, CCM imewapongeza Watanzania bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kwa kushiriki kwa amani na utulivu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kwani ushiriki wao kwa pamoja, umeyafanya maadhimisho hayo yafane.