Na Dunstan Mhilu, Ruvuma
MUUNGANISHO wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kutoka kikundi cha ’Moto Moto’ kilichopo katika Kijiji cha Amani Makoro, Kata ya Mkako wilayani Mbinga, umepanga kuongeza hekari nyingi kadiri ya uwezo katika msimu huu wa kilimo hususani katika zao la alizeti na mhogo.
Taarifa hiyo ilitolewa hivi karibuni na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho ambaye pia ni mwana kikundi, Ndambwe Joseph na pia ameiomba MUVI kuendelea kuwaunga mkono kwa kila hatua kwani mwamko wao ni mkubwa katika eneo hilo. Alisema watu wameamua kulima zaidi baada yakusikia kuwa mashine ya kukamua alizeti imefungwa katika Kijiji cha Mkako kilichopo jirani na kijiji chao.
Naye, Paulo Ambrose Komba mmoja wa wanakikundi cha moto moto amesema wameshaanza kulima changamoto kubwa ni mbegu na pembejeo hivyo ameiomba MUVI kuwasaidia ili kufanikisha zoezi hilo.
”Tuna lima kwa bidii, changamoto kubwa ni mbegu za alizeti, tunaiomba MUVI ituwezeshe kama ilivyo tuwezesha mwaka jana kutupatia mbegu za alizeti na mhogo.
Akijibu maombi hayo, Mratibu wa MUVI, Ruvuma, Neema Munisi alisema taasisi yao haitawapa wana vikundi wa MUVI mbegu na pembejeo kama ilivyo fanya msimu wa kilimo uliopita kwani kwa kufanya hivyo vikundi hivyo havita simama na kujitegemea.
”Ifike mahali mjitegemee, kwa maana kwamba ukiwa umenunua mbegu, mbolea na madawa utakuwa na uchungu na utatunza zao la alizeti na mhogo, tofauti na kupewa kila kitu bure, hata hivyo hatuta acha kuwaunga mkono kwa kila hatua.
”Mwaka jana tuliwapatia pembejeo na mbegu za alizeti na mhogo msimu huu tuta wapatia mbegu za alizeti kwa asilimia 50 kwa kila mwana kikundi na vipandiyo vya mhogo robo heka kwa kila mwana kikundi sambasamba na lile shamba darasa lenu, hivyo basi mnapaswa mchangie asilimia 50. Asiye changia asilimia hiyo basi hata ile asilimia ya MUVI hatapatiwa tujenge dhana ya kujitegemea.” Alisema.
Wakati huo huo afisa kilimo wa Wilaya ya Mbinga, Cathbert Mwinuka aliye ambatana na afisa kilimo wa kata ya mkako Kalenga amewataka kuandaa mashamba mapema na kununua mbegu hizo mapema pamoja na hizo watakazo pewa na MUVI ili wasije pata hasara kama waliyopata msimu uliopita hali ya hewa imebadilika inabadilika.
Kilo moja ya mbegu ya alizeti mkoani Ruvuma huuzwa sh. 5000, wakati lita moja ya mafuta ikiuzwa shilingi 3500/= hadi 4000/= alizeti inayo uzwa Ruvuma hutoka Singida na Njombe hii ina ashiria kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa kulima alizeti katika mkoa wa Ruvuma. MUVI ipo kwa ajili ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la alizeti na mhogo mkoani Ruvuma na kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mhogo pamoja na alizeti.