Na Rajab Mkasaba, Dar es Salaam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuandaa mazingira mazuri ili Benki zinazota huduma kwa kufuata masharti ya Kiislamu ziwe kwenye wigo mmoja na Benki nyingine nchini.
Rais Dk. Shein ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa Tawi jipya la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) inayotoa huduma za kibenki kwa kuzingatia masharti ya Kiislamu, lililofunguliwa Mtaa wa Kariakoo Lumumba/Mahiwa jijini Dar es Salaam.
Katika maelezo yake Dk. Shein amesema kuna haja kwa Benki Kuu ya Tanzania kuweka mazingira mazuri ya kusimamia huduma za benki ya Kiislamu kama ilivyo kwa benki za kawaida.
Dk. Shein alisema kuwa kuanzishwa kwa tawi hilo katika mtaa wa Lumumba ni kielelezo kingine kinachoashiria jinsi Benki ya PBZ ilivyovinjari kueneza huduma zake na hivyo kushindana na benki nyingine hapa Tanzania na kwingineko.
Aidha amesema tawi hilo la Benki ya PBZ jijini Dar es Salaam ni la tatu kati ya matawi yake yanayotoa huduma ya Benki ya Kiislamu ambapo moja katika hayo liko ChakeChake Pemba, jengine lipo Unguja.
Dk. Shein alisema kuwa huduma zinazotolewa na Benki hiyo ni huduma za Benki ya Kiislamu ambazo zinaendana na mfumo mzima wa Kiislamu ambapo katika kutoa huduma hiyo riba hairuhusiwi.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisisitiza kuwa Benki ya Kiislamu haziwazuii wateja wengine ambao sio Waislamu kujiunga ambapo pia, huduma zake hutolewa kwa watu wote bila ya kujali dini au tofauti nyengine yoyote.
Akitolea mfano nchi ya Malaysia, Dk. Shein alisema kuwa asilimia 60 ya wateja wanaotumia huduma hizi si Waislamu, hivyo aliwasihi wananchi kutumia huduma hizo ambazo zinatolewa bila ya ubaguzi wowote.
“Benki ya Kiislamu ni huduma mpya kwa maana ya kuwa hazijasambaa ipasavyo na bado kujulikana na wananchi wengi wa Tanzania hivyo natoa nasaha zangu kwa Uongozi wa Benki ya PBZ kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania juu ya huduma hii na kueneza huduma hizi sehemu nyenginezo za Tanzania”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa Benki ya PBZ kuangalia maendeleo yanayofikiwa katika huduma hizo sehemu nyengine duniani ili waweze kukidhi ipasavyo mahitaji ya wateja wao pia, wawe washindi katika ulimwengu huu ambapo ushindani wa Kibenki unazidi kuwa mgumu siku hadi siku.
Hata hivyo, Dk. Shein aliutaka uongozi wa PBZ kuangalia uwezekano wa kufunguwa matawi yao katika mikoa mengine kama vile Tanga, Arusha, Mwanza na kwengineko lakini aliwasihi kufanya utafiti kwanza kabla ya kufungua matawi hayo.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa PBZ kwa hatua nzuri ya kuimarisha huduma zao na kutanua biashara zao.
Pia, Dk. Shein alitoa wito kwa yale matawi yanayoendeshwa kwa mfumo wa kutoza riba, waangalie uwezekano wa kuweka viwango nafauu kwa wateja wao ili wavutike kwa wigi katika kuchukua mikopo ya aina mbali mbali na kuweza kuendesha maisha yao.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mhe. Omar Yussuf Mzee alisema kuwa takwimu zinazonesha kuwa Tanzania ina jumla ya watu milioni 42 lakini watu wanaotumia huduma za benki hawazidi milioni tano, hivyo kutokana na changamoto hiyo pia, ni miongoni mwa sababu iliyoifanya PBZ kuongeza kufungua matawi yake.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Juma Amour alieleza kuwa huduma za Benki ya Kiislamu zimesambaa katika nchi mbali mbali duniani zikiwemo Singapore, Thailand, Australia, Malaysia na nchi nyenginezo.
Alieleza kuwa rasilimali za mabenki ya Kiislamu ulimwenguni zimeongezeka kutoka dola za kimarekani 150 bilioni mwaka 1990 hadi kufikia Dola za Kimarekani trilioni moja mwaka 2010, ambapo inakisiwa kwamba ifikapo mwaka 2015 kutakuwa na kiasi cha rasiliamli zipatazo Dola za Kimarekani trilioni tano.
Alieleza kuwa ashughuli kubwa inazofanywa na benki hiyo ya Kiislamu ni pamoja na kupokea amana za wateja chini ya akauti ya akiba ya amana, akaunti ya akiba ya uwezeshaji, akaunti ya Hundi ya amana, Akauni ya uwekezaji, akaunti ya uwekezaji ya muda maalum na kutoa mikopo ya aina mbali mbali.
Akiitaja mikopo hiyo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa ni pamoja na mikopo kwa njia ya Murabah, mikopo kwa njia ya Bai muajjal na kueleza kuwa mikopo kwa njia ya Ijara na musharaka itaanza hapo baadae.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mtendaji alieleza kuwa nia ya benki hiyo ya PBZ hapo baadae ni kueneza huduma ya vituo vya benki sehemu mbali mbali, kutanua wigo wa huduma kwa mfano kuanzisha bima ya Kiislamu(Tkaful), Usimamizi wa mradi na huduma nyenginezo.