‘Mwanaume’ Tusker Chalenji ajulikana

Baadhi ya wachezaji wa Uganda wakishangilia mara baada ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuwakabidhi Kombe la Ushindi wa Kombe la Mashindano ya CECAFA Tusker Chalenji leo Dar es Salaam.

Shangwe, nderemo na madoido yakiendelea uwanjani mara baada ya washindi kukabidhiwa kombe.

Baadhi ya viongozi na wadhamini wakuu wa Kombe la Tusker Chalenji wakipiga picha ya pamoja huku wachezaji wa Uganda wakishangilia baada ya kukabidhiwa mwali.

*Ni Timu ya Taifa ya Uganda, yatwaa Kombe na USD 30,000

Na Joachim Mushi

HAYAWI hayawi! sasa yamekuwa, hatimaye kidume wa Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji linalodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Ltd (SBL) amejulikana leo katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Kidume ni Timu ya Taifa ya Uganda ambayo imefanikiwa kuing’oa Timu ya Taifa ya Rwanda kwa mikwaju ya penati baada ya kucheza kwa dakika 120 bila kupatikana mshindi.

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Uganda wakilionesha kombe


Timu ya Taifa ya Uganda imefanikiwa kuifunga Rwanda mabao 5-4 pamoja na magoli ya mikwaju ya penati iliyopigwa kwa kila timu penati tano tano. Mpira wa leo ulikuwa mkali, wenye kasi, ushindani mkubwa kiasi cha kuleta mvuto wa pekee kwa mashabiki.

Rwanda ndiyo walikuwa wa kwanza kuifunga Uganda baada ya kuanza kwa kipindi cha pili cha mchezo ambapo katika dakika ya 50 mchezaji wao Kagere Medie aliandika bao la kwanza kwa shuti kali ndani ya boksi la golikipa Abby Dhaira wa Uganda na kuandika bao la kwanza.

Baada ya goli hilo Uganda walikuja juu na kulishambulia lango la Rwanda na dakika ya 76 ya mchezo walisawazisha kupitia kwa mchezaji wao Isaac Isinde jambo ambalo liliufanya mchezo huo kuongeza kasi zaidi.

Iliwachukua dakika chache vijana wa Rwanda kulisakama lango la Uganda na katika dakika ya 78, mchezaji hatari Medie tena aliandika bao la pili na kuifanya timu yake kuongoza. Naweza kusema ilikuwa funga nikufunge katika mchezo huo uliokuwa na ushindani.

Uganda walilishambulia lango la wapinzani wao mara kwa mara na ilichukua dakika 2 tu na hatimaye kusawazisha bao hilo kupitia kwa mchezaji wao Hamis Kiiza katika dakika ya 80 ya mchezo.

Baada ya kusawazisha bao hilo, timu ya Uganda ilionekana kuwa na nguvu zaidi ambapo waliendelea kuliandama lango la wapizani wao mfululizo huku Rwanda wakijihami zaidi na kufanya mashambulio ya kushtukiza. Hadi zinakamilika dakika 90 timu zote zilikuwa suluhu 2-2.

Mwamuzi Wiish Yabarow kutoka Somalia alilazimika kuongeza dakika 30 ili kumpata Bingwa wa Kombe hilo, ambapo Rwanda walionekana kuelemewa na Uganda ndani ya dakika hizi-lakini hadi zote zinamalizika hakuna timu iliyoweza kubadili matokeo ya awali hivyo kuingia kwenye mikwaju ya penati tano tano kwa kila timu.

Katika mikwaju ya penati Rwanda iliambulia penati 2 huku Uganda ikijipatia penati 3, hivyo Uganda kutawazwa mabingwa wa KOMBE LA CECAFA TUSKER CHALENJI 2011, kukabidhiwa kombe pamoja na Dola 30,000 za Kimarekani na medali za dhahabu. Mshindi wa Pili Rwanda amejipatia Dola 20,000 na medali za shaba na Timu ya Taifa ya Sudan ambayo iliifunga Tanzania 1-0, katika mchezo wa kwanza kumtafuta mshindi wa tatu, imejipatia Dola 10,000 na medali za fedha.

Mabingwa watetezi Tanzania wameambulia patupu, baada ya kushindwa angalau kujitetea mbele za Watanzania hivyo kujikuta wakipata kipigo cha goli moja na kwa mtungi dhidi ya Sudan.