Waziri Pinda azindua mradi wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika

Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda

Na Mwandishi Maalum

MRADI wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika wenye kuenzi mchango wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika katika harakati za ukombozi wa Bara hilo, umezinduliwa jijini Dar es Salaam Alhamisi Des. 8, 2011 na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Chini ya mradi huo, kumbukumbu, alama, nyaraka , maarifa na taarifa mbalimbali kuhusu harakati za ukombozi zitakusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya saa na vizazi vijavyo ikiwa ni pamoja na kutambua waliojitoa mhanga kwa ukombozi.

“Hii ni nafasi ya kuwaumbua wasioutakia mema umoja wa Afrika wanaodai kuwa hatukuwahi kufanya jambo lolote kujisaidia wenyewe kwa wenyewe katika suala la ukombozi na changamoto nyingine,” Pinda alisema katika hotuba yake kabla ya uzinduzi wa mradi huo.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Pinda aliondoa pazia kwenye bango lenye nembo na lilioandikwa “The African Liberation Heritage Programme” (Mradi wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika), kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani City.
Tanzania imeteuliwa kuwa mahali pa kuanzishia mradi huo kutokana na mchango wake mkubwa katika ukombozi na kutokomeza tawala za kibaguzi Kusini mwa Afrika. Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Afrika yalikuwa Dar es Salaam kwa miaka yote 30 ya uhai wa Kamati hiyo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU, hivi sasa AU), Brigedia Hashim Mbita, pia alishiriki.