SMZ kudhibiti ufujaji Airport Zanzibar

Sehemu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali imeamua kujenga Uwanja wa ndege wa Zanzibar kwa lengo la kukuza uchumi, huku akiweka bayana taratibu zinazochukuliwa kudhibiti ufujaji mapato kiwanjani hapo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya ziara yake ya kutembelea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ambapo alitembelea kituo cha Zimamoto, sehemu ya mizigo iliyosimamiwa na ZAT, VIP, sehemu ya abiria wanaoingia na kutoka nchini, smaegesho ya gari, ujenzi wa jengo jipya la abiria na kuangalia uzio pamoja na barabara ya kurukia na kutulia ndege.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa uwanja wa ndege wa Zanzibar una changamoto kubwa katika ukukuza uchumi hivyo mashirikiano yanahitajika katika ukusanyaji wa mapato ili yasivuje.

Dk Shein alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo ndio maana serikali imeamua kwa makusudi kujenga jengo jipya la abiria na sehemu nyenginezo ikiwemo barabara ya kurukia na kutulia ndege ili kuweza kutua ndege za aina zote kutoka sehemu mbali mbal kwa lengo lilelile la kkuza uchumi wa Zanzibar.

Alisema kuwa kuna kila sababu kwa kila mdau na mfanyakazi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar kushirikiana na serikali ili kuweza kukusanya mapato yatakayosaidia maendeleo nchini.

Dk Shein aliwataka wadau wote kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali na kila mmoja afanye kazi zake kwa sheria na taratibu zilizopo na kusisitiza kwua tayari kwa upade wa serikali imejipangia mikakati madhubuti na imeanza kufanya vizuri.

“Sisi serikalini hatuna lengo la kumtia adabu mtu badala yake tuna lengo la kutengeneza na kukiimarisha kiwanja chetu cha ndege ili kiimarike zaidi na zaidi na kuweza kuyavutia mashirika mengine ya ndege duniani yalete ndege zake,” alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Uhamiaji kiwanjani hapo pamoja na uongozi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar kukaa pamoja katika kuziangalia changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma kwa wasafiri kutokana na kuwemo malalamiko kadhaa juu ya utoaji huduma kwa wageni.

Dk. Shein alitoa wito wa kuuendeleza na kuuimarisha uwanja huo wa ndege uweze kutoa huduma bora ili jina lake ambalo ni jina la kiongozi wa mwanzo wa Zanzibar liweze kusibu na kuenziwa kutokana na juhudi zake katika kuleta maendeleo endelevu nchini.

Alisema kuwa tayari mashirika kadhaa duniani yameshaazimia kuleta ndege zake hapa Zanzibar likiwemo Shirika la ndege la Qatar, Turkey, Emirate, Arabia na mengineyo, hivyo aliwataka wadau na wafanyakazi wa uwanja huomwa ndege wabadilike katika utendaji wao wa kazi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ni azma ya serikali kuufanya uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kuwa ni eneo la biashara zinazokwenda nje ya nchi (EPZ) na kusisitiza kuwa serikali imeamua kuekeza fedha nyingi sana ambazo ni zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la uwanja huo

Hata hivyo, Dk. Shein alipongeza na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar katika uwanja huo wa ndege hatua ambayo itasaidia kutoa huduma kwa ufanisi zaidi. Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa lengola serikali ni kuhakikisha uchumi unaimarika kwa kuweza kuingiza wageni wengi.

Mapema kabla ya ziara yake Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Miundombinu a Mawasiliano ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Alielezwa kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na matengenezo ya njia ya kutulia na kutrukia ndege, mradi wa ujenzi wa uzio, ujenzi wa jengo jipya la abiria na ukarabati mkubwa wa taxiway zilizopo na apron na kujenga nyengine mpya.

Aidha, Rais alielezwa kuwa ujenzi wa jengo jipya la abiria ambalo linajengwa kutokana na mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani 70.4 kutoka Benki ya Exim ya China unatarajiwa kumalizika mwaka 2013.

Alielezwa kuwa ujenzi huo unatekelezwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya China, ambapo pamoja na jengo hilo Mkandarasi anajenga eneo la kuegesha ndege apron lenye ukubwa wa mita za mraba 33,000, eneo la kuegesha magari mbele ya jengo hilo yapatayo 163 kwawakati mmoja.