*Yachapwa 3-1 na Waganda, mashabiki Yanga washerekea
Na Joachim Mushi
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars jana imetolewa kuingia fainali katika Mashindano ya Kombe la Tusker baada ya kukubali kichapo cha mabao 3 kwa moja (3-1) kutoka kwa majirani zao wa Uganda.
Kwa matokeo hayo Tanzania imeshindwa kutetea Ubingwa ambao ilikuwa ikiushikiliwa wa kikombe hocho cha CECAFA Tusker Chalenji, na sasa inalazimika kukutana na timu ya Taifa ya Sudan Desemba 10 kutafuta mshindi wa tatu wa kombe hilo.
Katika mchezo huo ambao ulionekana kuwa wa upande mmoja baada ya kikosi cha stars kuonekana kuzidiwa maeneo yote huku kikimtegemea mchezaji mmoja Mrisho Ngassa. Tanzania ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Mrisho Ngassa, baada ya kupokea pasi ndefu toka kwa Ramadhan Chombo Ridondo na kumtoka gilikipa kabla ya kushinda kirahisi. Hadi timu zinakwenda mapumziko Tanzania ilikuwa na goli moja huku Uganda ikiambulia patupu.
Baada ya kuanza kwa kipindi cha pili vijana wa Uganda walikuja juu na hatimaye dakika ya 55, mchezaji Andrew Mwesigwa aliisawazishia timu yake kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Sula Matovu.
Baada ya kusawazisha vijana wa Kiganda walionekana kuamka zaidi na kucheza kwa hari kiasi cha kuifanya vijana wa Tanzania kuonekana wamepwaya na kuridhika na hali halisi. Hadi dakika 90 zinamalizika timu zote zilitoka suluhu ya 1-1, hivyo kuongezewa dakika 30 ili kumtafuta mbabe.
Uganda ilipata goli la pili katika dakika ya 101, likifungwa na Emmanuel Okwi, goli lililowapa nguvu zaidi na kuendelea kulisakama lango la Tanzania. Ndoto za kuingia fainali kwa Kilimanjaro Stars ya Tanzania zilitoweka kabisa mnamo dakika ya 112, baada ya mchezaji wa Uganda Isaac Isende, kufunga goli la tatu kwa njia ya penati iliyosababishwa na Juma Nyoso aliyemuangusha Okwi eneo la hatari.
Kwa matokeo hayo sasa Timu ya Taifa ya Uganda itaingia uwanjani Jumamosi kuivaa timu ya Taifa ya Rwanda, katika fainali za michuano hiyo ya Kombe la Tusker Chalenji. Rwanda imeingia hatua hiyo baada ya kuichapa Sudan mabao mawili kwa karai. Mabao ya Rwanda yamefungwa na Iranzi Jean dakika ya 5 na lingine dakika ya 77, huku Sudan ikijipatia goli pekee dakika ya 69 ya mchezo kupitia kwa Mohamed Mussa.
Timu ya Taifa ya Uganda ilikuwa ya kwanza kukata tiketi ya kuingia fainali ya Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji yanayoendelea jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania. Uganda imeingia fainali ya michezo hiyo baada ya kuichapa timu ya Taifa ya Sudan magoli 2-1, katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliozikutanisha timu za Uganda na Sudan.