Na Magreth Kinabo–MAELEZO
SERIKALI imesema msongamano wa ndege zinazosubiri kutua au kuruka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere umepungua baada ya kuufanyia ukarabati mkubwa uwanja huo ambao umeongeza uwezo wa kuhudumia ndege 30 kwa saa badala ya nane.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu katika sherehe ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya usafiri wa anga duniani zilizofanyika kwenye viwanja vya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TAA) jijini Dar es Salaam. Ambapo kauli mbiu yake ni ‘Kusaidiana na Kushirikiana kwa ajili ya Usafiri Endelevu wa Anga Duniani’.
“Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania imekamilisha matengenezo makubwa ya miundombinu na uboreshaji wa mitambo…Mategenezo haya yamejumuisha ukarabati mkubwa wa njia ya kurukia ndege, viungio vyake na maegesho ya ndege,” alisema Waziri Nundu.
Waziri Nundu aliongeza kuwa Serikali itaendeleza juhudi za kuboresha miundombinu na ubora wa huduma za usafiri wa anga katika viwanja vya ndege nchini hadi viwepo vya kutosha vya kuweza kuhudumia nchi nzima. Hivyo kwa kuanzia Serikali imepanga kushughulikia viwanja 17.
Aliongeza kuwa ili usafiri huo uwe endelevu, uwepo wa wataalam wa usafiri wa anga ni muhimu. Serikali itashirikiana na mamlaka hiyo na wadau wengine kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanapata mafunzo hayo.
Aidha Waziri Nundu alisema hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa katika suala hilo kwa kuwa marubani na wahandisi wengi wazalendo wana umri wa miaka zaidi ya 50, ambapo aliishauri mamlaka hiyo na wadau kuanza taratibu za kuimarisha mfuko wa mafunzo huku akiutaka uwe endelevu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Fadhili Manongi alisema idadi ya abiria wanaotumia usafiri huo imeongezeka kutoka 1,206,821 mwaka 2000, hadi abiria 3,027,512 mwaka 2010 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 151.
Alisema safari za ndege pia zimeongezeka kutoka 112,821 hadi 181,240 katika kipindi hicho kwa asilimia 61 na kuhusu utalii nchi ilipokea 782,699 kwa mwaka 2010 ukilinganisha na watalii 501,669 mwaka 2000.
Manongi aliongeza kuwa asilimia 50 au 60 ya watalii hutumia usafirihuo na iliyobakia wa barabara hawa wanaotoka nchini Kenya baada ya kuwasili kwa ndege nchini humo.