Nusu Fainali CECAFA Tusker Chalenji kesho

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Serengeti Breweries (SBL), Phraim Mafuru akitoa ufafanuzi kuhusiana na SBL kuendelea kudhamini Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji hata kama yatafanyika nje ya Tanzania hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu

MECHI mbili za nusu fainali kuwania ubingwa wa 35 wa michuano ya CECAFA Tusker Challenge Cup inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) zinachezwa kesho (Desemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, jijini Dar es Salaam na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura imesema nusu fainali ya kwanza ni kati ya Rwanda na Sudan itachezwa kuanzia saa 8.00 mchana na kufuatiwa na ile ya pili kati ya mabingwa watetezi Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na Uganda (The Cranes) itakayoanza saa 10.00 jioni.

Wambura amesema viingilio katika mechi hizo ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B, n ash. 20,000 kwa VIP A.

Alisema mechi ya fainali na ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Desemba 10 mwaka huu. Bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) atapata dola za Marekani 30,000, makamu bingwa dola 20,000 na mshindi wa tatu dola 10,000.

Wakati huo huo, Wambura amesema timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) iliyoko Gaborone, Botswana kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) inatarajia kurejea nchini Desemba 9 mwaka huu.

Amebainisha Ngorongoro itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam saa 10 alfajiri kwa ndege ya PrecisionAir. Timu imeshindwa kupata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye kundi lake la C.

Mabingwa watetezi Zambia ndiyo walioongoza katika kundi hilo kwa kuizidi Ngorongoro Heroes kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Ngorongoro ilicheza mechi tatu ambapo ilitoka sare na Zambia na Afrika Kusini na baadaye kuifunga Mauritius mabao 3-0. Kila kundi lilikuwa linatoa timu moja kuingia hatua ya nusu fainali itakayochezwa Desemba 8 mwaka huu na baadaye fainali Desemba 10 mwaka huu.

Timu zilizofuzu kucheza nusu fainali ni mabingwa watetezi Zambia, wenyeji Botswana, Malawi na Angola. Nchi nyingine zilizoshiriki michuano hiyo ni Msumbiji, Madagascar, Zimbabwe, Swaziland, Lesotho, Namibia, Comoro na Seychelles.