Na Ngusekela David, Tanga
MRADI wa Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) umetoa mafunzo mbalimbali kwa wajasiriamali ili kuhakikisha inawajengea uwezo katika shughuli zao za kila siku na hatimaye kujikwamua kwenye lindi la umasikini.
Mafunzo hayo yanayojulikana kama mafunzo ya ‘Ujasiriamali na Uongozi wa Biashara’ yamefanyika wilayani Handeni huku yakihusisha wakulima, mawakala wa pembejeo, wasindikaji pamoja na wadau anuai wa mnyororo wa thamani wakiwemo maofisa kilimo na watoa huduma za kibiashara.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni pamoja na ujasiriamali, kuelewa mazingira ya biashara na Kuelewa soko na huduma kwa mteja nyingine ni Kumbukumbu za biashara na usimamizi wa fedha na Mipango na mikakati endelevu ya biashara.
Mafunzo hayo yaliodumu kwa siku tano yaani Novemba 28, hadi Desemba 2 yalifungwa na Meneja wa SIDO, Mkoa wa Tanga, Suleimani Mtany na yanatarajiwa kuwa chachu kwa wajasiriamali katika kujikwamua na umasikini.
Akifunga mafunzo hayo, Mtany aliwasihi washiriki kutumia vizuri elimu walioipata kwani taasisi ya MUVI kwa kushirikiana na SIDO watakuwa bega kwa bega kuhakikisha kuwa wanapata huduma wanazohitaji kirahisi, ikiwa ni pamoja na soko, teknolojia mpya na vinginevyo.
Aidha aliongeza kuwa washiriki wanapata fursa ya kutembelea maonesho mbalimbali pindi yanapotokea kwani ni njia pekee ya kujifunza vitu vingi zaidi kwa muda mfupi.
Katika hatua nyingine Mkufunzi wa Mafunzo hayo kutoka Kampuni ya Richland alitoa rai kwa washiriki kujijengea tabia za kijasiriamali kwani huwezi kufanikiwa pasipo kuwa na dhamira ya dhati ya kufanya kile unachokifanya.
Amesema njia pekee ya kufanya biashara kuwa ya kudumu ni kutunza kumbukumbu na kuwa na mpango mkakati unaoonyesha ulikotoka, ulipo na ni wapi uendako, hii inamsaidia mjasiriamali kukubalika hata katika taasisi za fedha na kuweza kukopesheka.
Mradi wa MUVI mkoani Tanga unatekelezwa na kampuni ya Match Marker Associate na kusimamiwa na SIDO chini ya udhamini wa shirika la kimataifa la maendeleo ya kilimo (IFAD).