Serengeti Breweries yadhamini pambano la wabunge Vs Wawakilishi

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Serengeti Breweries Ltd (SBL), Teddy Mapunda (wa pili kushoto) akimkabidhi Nahodha wa Timu ya Bunge la Tanzania, Amos Makala (Mb) vifaa vya michezo kwa timu yao vitakavyotumika katika pambano kati ya timu hiyo na ya Balaza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Joachim Mushi)

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Serengeti Breweries Ltd (SBL), Teddy Mapunda (wa pili kushoto) akikabidhi kombe litakaloshindaniwa na timu zote mbili kwa viongozi wa Timu za Bunge la Tanzania na lile la Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Timu ya Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma na kushoto ni Nahodha wa Timu ya Bunge, Amos Makala (Picha na Joachim Mushi)

*Pambano kufanyika 9 Desemba kati ya Wabunge na Wawakilishi

Na Joachim Mushi

KAMPUNI ya Serengeti Breweries Ltd (SBL) imetangaza udhamini wa pambano la kihistoria la mpira wa miguu na wa mikono ‘netball’ kati ya timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania na ile ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) Zanzibar.

Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ofisi za kampuni ya SBL ambapo pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL, Teddy Mapunda amekabidhi vifaa vyote muhimu vya michezo kwa timu zote mbili.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mapunda alisema SBL kupitia kinywaji chao kilichojinyakulia tuzo mbalimbali za ubora cha bia ya Serengeti wamedhamini pambano hilo kwa fedha takribani milioni 65.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Serengeti Breweries Ltd (SBL), Teddy Mapunda (katikati) akiwakabidhi kombe la mpira wa netibali Ofisa Michezo wa BLW, Dau Hamad Maulid (kushoto) na Nahodha wa Timu ya Netibali ya Bunge la Tanzania, Mkiwa Kimwanga (kulia).


Amesema udhamini huo umejumuisha vifaa vya michezo kwa timu za mpira wa miguu kwa pande zote, pamoja na mpira wa mikono kwa wanawake, ambapo wametoa jezi kwa timu zote, viatu, vifaa vingine vya michezo pamoja na malazi kwa timu kukaa kambini.

Mapunda amesema mechi hizo zitakazochezwa siku ya maadhimisho ya sherehe za uhuru mwaka huu, mara baada ya shughuli za maadhimisho katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam baadaye itafuatiwa na hafla fupi jioni kwa kukutanisha pande zote na kubadilishana mawazo.

“Kwa kawaida ulimwenguni, michezo hutumika kuunganisha watu, michezo pia huwaleta watu karibu. Serengeti Breweries tupo katika mstari wa mbele katika kuendeleza michezo. Tunadhamini timu ya taifa kupitia kinywaji cha Bia ya Serengeti na Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji yanayoendelea jijini Dar es Salaam,” alisema B. Teddy Mapunda.

Alisema mshindi katika mchezo huo atapata kikombe pamoja na medali za dhahabu kwa timu zote mbili, mpira wa miguu na netibali huku mshindi wa pili ataambulia medali za fedha.

Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo viongozi wa timu zote wametambiana, huku kila mmoja akidai atamwadhibu vibaya mwenzake katika mchezo huo ambao wamedai utadumisha mshikamano na muungano wa Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar).

Mwenyekiti wa Timu ya Baraza la Wawakilishi (BLW), Hamza Hassan Juma amesema wao wapo kambini tangu Novemba 30, mwaka huu eneo la Nungwi wakijifua kwa pambano hilo ambalo amedai ni lazima watashinda ushindi mnono.

Kwa upande wa Timu ya Bunge la Tanzania, Nahodha wa timu hiyo, Amos Makala ametamba wao hawajawahi kufungwa katika michezo yao yote hivyo hawawezi kuvunja mwiko huo. Amewashauri wapinzani wao wajiandae kuzuia wingi wa magoli kwani wanahasira za kuhujumuwa katika mashindano ya mabunge yaliyomalizika hivi karibuni.

Aidha amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kushuhudia mpambano huo ambao hautakuwa na kiingilio chochote kwa watanzamaji.