TAFFA kuondoa urasimu bandarini

Baadhi ya shehena ya magari yakiwa yamelundikana katika bandari ya Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) kinacho shughulikia shehena zote zinazo ingia na kutoka nchini kwa njia ya bandari, anga na mipakani kimesema kimepanga kujenga ushirikiano na taasisi anuai inazofanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha inaongeza na kuinua pato la Serikali kupitia shughuli zao.

Kauli hiyo imetolewa jana na rais wa chama hicho, Stephen Ngatunga alipokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam. Rais huyo wa TFFA, amesema atahakikisha shughuli zote za kiutendaji zinafanyika kwa ufanisi na kwa wakati ili kuondoa usumbufu eneo hilo.

Pamoja na hayo ameongeza kuwa chama hicho kimepanga kujenga ushirikiano mzuri na taasisi anuai inazofanya kazi kwa pamoja zikiwemo; TRA, TPA, TICTS, ICD’S na Shipping Line ili kuongeza pato la taifa kupitia Mamlaka ya Bandari nchini.

Aidha, Ngatuma amesema kwa kushirikiana na taasisi hizo watahakikisha wanalinda heshima ya Bandari ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Majini na Nchi kavu (SUMATRA) ili kuondoa sera zote za kirasimu zinazo changia ucheleweshwaji wa uondoshwaji wa shehena bandarini.

Katika hatua nyingine TAFFA imepanga kuanzisha chuo kitakacho endesha mafunzo kwa njia ya mitaala inayofundishwa na chuo cha TRA kuanzia Januari 2012 na kutoa fursa kwa wahitimu kufanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).