Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ramadhani Dau kutokana na kifo cha Mwandishi wa Habari Mkongwe, Alfred Ngotezi aliyekuwa akifanya kazi katika mfuko huo kama Ofisa Uhusiano Mwandamizi.
Ngotezi aliyewahi kufanya kazi katika gazeti la Serikali la Daily News kabla ya kuhamia mfuko wa NSSF, alifariki ghafal mjini Arusha alikokuwa amekwenda kikazi Desemba 3, 2011.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na kifo cha Alfred Ngotezi aliyekuwa mchapakazi hodari katika fani ya Uandishi wa Habari. Hakika kifo chake kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa familia yake bali pia katika jamii yetu kwa ujumla hususan katika taaluma yake ya Uandishi wa Habari,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ametoa pole nyingi kwa familia ya Marehemu Alfred Ngotezi na amewaomba wanafamilia wawe na uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo huku akiwahakikishia kwamba yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Aidha Rais Kikwete amesema Waandishi wa Habari kote nchini hawana budi kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Marehemu Ngotezi enzi za uhai wake hususan jitihada zake kubwa za kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi kupitia kalamu yake.