Na Mwandishi Wetu, Arusha
VIONGOZI mahasimu wa kisiasa mjini Arusha kutoka vyama vya CCM na CHADEMA juzi wamejikuta wakipeana mikono na kupatanishwa kanisani na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kwenye hafla ya harambee.
Viongozi waliopatanishwa ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema pamoja na Meya wa Manispaa ya Arusha Gaudance Lyimo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Sitta ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, alilazimika kufanya zoezi hilo baada ya kuombwa afanye hivyo na Lema katika harambee ya Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresa ambapo viongozi hao walikutana.
Katika mazungumzo yake Lema aliweka bayana kuwa hajawahi kukaa meza moja na Meya huyo, kitendo ambacho hakioni kizuri katika shughuli zao za kazi. Aliongeza kuwa kimsingi hana kinyongo na Meya huyo bali namna ya alivyochaguliwa, jambo ambalo alidai lilikiuka sheria.
Akizungumza, Meya Lyimo, alibainisha kuwa Kanisani si mahali pa
kuzungumzia masuala ya siasa na kutaka jambo hilo waachiwe madiwani kwani ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua.
Hata hivyo baadaye Waziri Sitta aliwaita mbele na kuwashikanisha mikono kwa ishara ya mapatano kati ya Lyimo na Lema.
“Kwa kuwa natambua kazi yetu ni kuwatumikia wananchi ambao ndiyo
wametuchagua ndiyo maana nimekubali kushikana mkono na Lema pamoja na ubaya wote alionifanyia Lema kwa sababu Waziri Sitta ndiye aliyenifanya nishikane mkono naye na nisingependa kutenda dhambi kwa vile tupo mbele ya Baba Askofu,” alisema Lyimo.
Mgogoro wa Umeya wa Manispaa ya Arusha umedumu takribani mwaka mmoja ambapo ulisababisha CHADEMA kuwavua uanachama madiwani wake watano akiwemo aliyekuwa Naibu Meya baada ya kusaini mwafaka wa uchaguzi wa mgogoro huo.
Akizungumza Sitta alisema mfumo wa vyama vingi hauna maana ya uhasama kwani wananchi wanapenda kuona viongozi wakishirikiana, wakitumia fursa ya uongozi waliyonayo kuharakisha maendeleo na si vinginevyo.
“Hizi ni nasaha za bure za kuwafanya CHADEMA waangalie suala hili, wapunguze ukorofi, unajua Lema baadhi ya watu vijijini wameanza kuwashangaa kwa sababu mbinu za harakati mnazotumia ikiwemo maandamano ziyo sahihi kwani Watanzania hawajazoea,”
“Chama kinachotarajia kuwa na madaraka kinatakiwa kianze kufanafana na Serikali, hakiwezi kuwa cha migomo wala maandamano, kwani huo ndio ushauri wangu kwenu iwapo mtaufuata utawasaidia, mkiupuuza mtaendelea kupata kura za mijini, kwani nguvu mnazozitumia hazitawafikisha mbali,” alisisitiza Waziri Sitta.
Aidha Harambee hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu akisaidiwa na Paroko Dk. Vincent Mhina na Padri Festus Mangwangi. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu alichagia milioni 10, Sitta milioni 1, na kuwasilisha pia michango mingine ya viongozi waliomuunga mkono. Sitta alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda amechanga milioni 5, Fredrick Sumaye milioni 1, Ismail Rage milioni 1, Hamisi Kigwangala milioni 1, Lema milioni 1 na Meya wa Arusha milioni 2.