Robo fainali Kombe la CECAFA Tusker Challenge leo

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Serengeti Breweries Ltd (SBL), Richard Wells (kulia) ambao ni wadhamini wakuu wa Michuano ya Tusker Chalenji kupitia bia ya Tusker akitoa ufafanuzi kuhusiana na udhamini wao.

MICHUANO ya Robo fainali Kombe la CECAFA Tusker Chalenji inaanza leo Desemba 5,2011 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura jana kwa vyombo vya habari leo zitapigwa mechi mbili mfululizo.

Wambura amesema mechi hizo mbili ambazo zitafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mchezo wa kwanza utafanyika majira ya saa 8.00 mchana kati ya Burundi na Sudan wakati ya pili utafanyika saa 10.00 jioni kati ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) dhidi ya Rwanda.

Aidha wambura amesema michezo hiyo itaendelea keshokutwa, yaani Desemba 6 mwaka huu, mechi ya kwanza ya robo fainali itakuwa kati ya Uganda na Zimbabwe wakati ya pili itakuwa saa 10.00 jioni kati ya mabingwa watetezi Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na Malawi (The Flames).

“Mechi zote zitaoneshwa moja kwa moja kupitia SuperSport 9. Viingilio kwa mechi zote za robo fainali ni sh. 2,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B na sh. 15,000 kwa VIP A.