Na Mwandishi Wetu
MTENDAJI Mkuu wa Mamlaka ya Barabara za Taifa (TANROADS), Injinia Patrick Mfugale amefanya mabadiliko makubwa kwenye safu ya uongozi ya TANROADS katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo amesema mabadiliko hayo yamelenga kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya barabara hasa mikoani.
Amesema mameneja walioteuliwa mikoani sasa watawajibika kusimamia ubora wa kazi, kukamilika kwa miradi ya maendeleo ndani ya muda wa mkataba hasa kwa miradi inayohusu mikoa yao na kuhakikisha kuwa thamani ya fedha zilizotumika ‘value for money’ inaendana na kazi husika.
Ntemo amesema katika mabadiko hayo kuna mameneja saba wapya, mameneja watano wamehamishwa vituo, mameneja wanne wakiteuliwa katika mikoa mipya na mameneja tisa wakiwa wamebaki katika vituo vyao vya zamani.
Alisema mameneja saba wapya walioingia katika uteuzi huo ni pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam, Injinia Julius Ndyamukama ambaye anachukua nafasi ya James Nyabakari aliyehamishiwa Mbeya- huku Injinia Lucian Kileo aliyekuwa Mbeya anahamishiwa Tanroads Makao Makuu.
Alisema Mkoa wa Kilimanjaro ameteuliwa Injinia Mwita Marwa Rubirya akitokea Wizara ya Ujenzi Makao Makuu, Naye Injinia Tumaini Sarakikya aliyekuwa Meneja wa mkoa huo amehamishiwa mkoa wa Pwani, huku Injinia Isaac Mwanawima amehamishiwa mkoa wa Lindi akitokea Makao Makuu.
Aidha alisema Injinia Dorothy Mtenga amepelekwa Morogoro akitokea TANROADS Dodoma na anachukua nafasi ya Injinia Charles Madinda ambaye sasa amehamishiwa TANROADS Makao Makuu. Kwa Mkoa wa Shinyanga amepewa Injinia Augustine Witonde Philip anayechukua nafasi ya Damian Ndabalinze ambaye amehamishiwa Tabora.
Mkoani Rukwa amehamishiwa Injinia Florian Kabaka anachukua nafasi ya Injinia Joseph Nyamhanga ambaye ameteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Barabara, Wizara ya Ujenzi. Nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Barabara ilikuwa wazi kufuatia kuteuliwa kwa Injinia Mussa Iyombe kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Aidha Injinia Isaack Kamwelwe amehamishiwa mkoa mpya wa Katavi akitokea Wizara ya Ujenzi Makao Makuu. Alisema mameneja watano waliohamishiwa mikoa mingine ni pamoja na Injinia Damian Ndabalinze anahamia Tabora akitokea Shinyanga. Injinia Tumaini Sarakikya amepelekwa Mkoa wa Pwani akitokea Kiliamnjaro.
Amesema Meneja TANROADS Mkoa wa Pwani Injinia Gabriel Mwikola amepelekwa Mtwara ambapo Injinia Mussa Mataka aliyekuwa Meneja wa mkoa huo amepangiwa Tanroads Makao Makuu.
Aidha mameneja wanne waliopangiwa mikoa mipya ni pamoja na Injinia Haruna Senkuku Mkoa wa Geita, Mkoa wa Katavi amepelekwa Injinia Isaack Kamwelwe, Mkoa wa Njombe amepangiwa Injinia Yusuf Mazana, Mkoa wa Simiyu amepangiwa Injinia Emanuel Kibeya.
Mameneja waliobaki katika vituo vyao ni Injinia Deusdedit Kakoko wa Mkoa wa Arusha, Injinia Leonard Chimagu wa Dodoma, Injinia Poul Lyakurwa wa Iringa, Injinia Johnny Kalupate wa Mkoa wa Kagera, Injinia Emmanuel Korosso Mkoa wa Mara, Injinia Yohani Kasaini wa Mkoa wa Mara, Injinia Leonard Kadashi Mkoa wa Mwanza, Injinia Yustaki Kangole Singida huku Mkoa wa Tanga amebaki Alfred Ndumaro.