Sabasaba
WIZARA ya Viwanda na Biashara imesema mchakato wa marekebisho sheria ya vipimo unaendelea kwa lengo la kutoa adhabu kali kwa wafanyabiashara wanaotumia vipimo ambavyo sio sahihi.
Hayo yamesemwa na Afisa Vipimo Mkuu daraja la pili, katika Wakala wa Vipimo Tanzania, Zainabu Kafungo katika maonyesho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Uwanja wa Mwalimu J K Nyerere Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Kafungo amefafanua kuwa hadi sasa tunapoadhimisha miaka 50 ya uhuru sheria za vipimo zilizopo zinatoa adhabu ndogo kwa wafanyabiashara wanaozikiuka kwa kutumia vipimo visivyosahihi, hivyo Wakala chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara wapo kwenye mchakato wa kuzifanyia sheria hizo marekebisho ili ziweze kutoa adhabu kali zaidi kwa wakiukaji.
“Kuna sheria zinazotoa adhabu kwa mfano ya shilingi za kitanzania 10,000/=, kiasi ambacho hakimuumi mtenda kosa,” ameeleza.
Ameeleza kuwa lengo la mchakato huo ni kurekebisha sheria, ili kuendelea kumlinda mlaji katika sekta za biashara, afya, usalama na mazingira kupitia matumizi ya vipimo sahihi na kuilinda jamii kutokana na matumizi mabaya yatokanayo na vipimo visivyo sahihi katika sekta hizo.
Afisa huyo ametaja baadhi ya mafanikio ambayo Wakala wa Vipimo wamepata wakati wa miaka 50 ya uhuru kuwa ni pamoja na kuongezeka vituo vya utoaji wa huduma na kusogezwa huduma hizo karibu zaidi na wananchi, hususani katika makao makuu ya mikoa yote Tanzania Bara na katika Wilaya zote za Dar es Salaam.
Pamoja na mafanikio hayo amebainisha baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na watumishi kuwa wachache kulingana na mahitaji halisi ya huduma na ukosefu wa vyombo maalum kwa ajili ya vipimo na maafisa ukaguzi ambao mara nyingine hutakiwa kusafiri na vipimo vyenye uzito wa hadi kilo 300.