Rais Kikwete amkumbuka marehemu Wakati

Marehemu David Wakati enzi za uhai wake.

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Tanzania, marehemu David Wakati.

Mzee Wakati aliaga dunia Desemba Mosi, 2011 kwenye Hospitali ya Regency kwa matatizo ya ugonjwa wa sukari. Katika salamu za rambirambi, Rais Kikwete amesema amesikitishwa na kuhuzunishwa juu ya taarifa za kifo cha Mzee Wakati kwa sababu alikuwa mtangazaji hodari, mzalendo, mwenye mapenzi kwa nchi yake na aliyetumia taaluma yake kwa ujenzi wa nchi.

“Nilimfahamu binafsi Mzee David Wakati. Alikuwa kielelezo cha utangazaji ulio bora katika nchi yetu na hata nje ya mipaka ya nchi yetu. Alikuwa mwana-taaluma hodari na aliyetumia taaluma yake vizuri kwa weledi na uzalendo katika ujenzi wa nchi hiyo. Ametoa mchango mkubwa kwa nchi hiyo na ameacha pengo kubwa kwa taaluma ya utangazaji.”

“Nakutumia wewe rambirambi, na kupitia kwako natuma rambirambi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu pamoja na wadau wote wa taaluma ya utangazaji. Napenda kuwahakikishieni nyote kwa dhati ya moyo wangu kuwa naelewa machungu yenu katika kipindi hiki kigumu lakini yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake kwa Mshana.

Amemalizia Rais Kikwete: “Aidha, napenda kuwahakikisheni kuwa moyo wangu uko nanyi katika wakati huu wa maombolezo, na msiba wenu ni msiba wangu. Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu Wakati. Amen.”