Bush ampongeza JK kwa huduma za afya!

Rais Jakaya Kikwete akipongezwa na Rais Mstaafu wa Marekani George W. Bush kwa sera nzuri za serikali yake kuhusu huduma za afya nchini hasa juhudi zinazofanyika kudhibiti malaria, Ukimwi na saratani Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ikulu)

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Desemba Mosi, 2011, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush ambaye yuko Tanzania kwa ziara ya siku sita.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wamezungumzia jinsi Taasisi ya Bush ‘Bush Institute for Global Health’ inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na changamoto za sekta ya afya na hasa magonjwa ya saratani.

Bush ambaye amefuatana na mkewe Mama Laura Bush amemweleza Rais Kikwete mipango ya taasisi yake katika kupambana na ugonjwa wa kansa ikiwa ni pamoja na jitihada za kupima, kuzuia na chanjo.

Aidha mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mama Salma Kikwete, Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kumweleza Bush jitihada za Serikali yake katika kupambana na magonjwa yanayoua watu wengi ikiwamo malaria, Ukimwi na saratani, magonjwa ambayo mapambano yake, Bush alichangia kifedha alipokuwa madarakani.

Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kumweleza, Bush kuhusu mipango mingine ya maendeleo inayosaidiwa na Marekani ikiwa ni pamoja na mpango mkubwa wa ujenzi wa miundombinu chini ya Mpango wa MCC. Rais Bush na familia yake wako katika ziara ya Afrika na mbali ya Tanzania wanatembelea pia Ethiopia na Zambia.