Mwanahabari Alfred Ngotezi afariki

TASNIA ya habari Tanzania imepata pigo kubwa baada ya jana kundokewa na mwandishi wa habari mkongwe, Alfred Ngotezi.
Taarifa zilizopatikana jana usiku zinaeleza kuwa Ngotezi, alidondoka muda mfupi baada ya kutoka maliwato, akiwa katika moja ya hoteli za Mji wa Arusha na alifariki dunia muda mfupi baadaye. Inaelezwa kwamba alifariki saa 5:11 usiku
“Ndugu yetu baada ya kurejea kutoka maliwatoni, akiwa ameketi na viongozi wake, alidondoka ghafla na kufariki dunia, kabla ya kuanguka na kufariki, Ngotezi aliomba kupigiwa wimbo mmoja, akacheza kwa furaha na kisha kupeana mikono na waimbaji wa bendi iliyokuwa ikitumbuiza hapo hotelini,” kilisema chanzo chetu cha habari kwa uhakika.
Ngotezi aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa NSSF hadi mauti yanamkuta, alikuwa Arusha kikazi kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa mifuko ya hifadhi ya jamii unaoanza Arusha kesho.
Mwanahabari huyo alikuwa mwajiriwa wa gazeti la serikali linalochapishwa kwa Kiingereza, Daily News kabla ya kuondoka na kuingia katika siasa ambako alithubutu kugombea ubunge, ingawa hakufanikiwa.
Hata baada ya kujiunga na NSSF, Ngotezi aliendelea kuwa mchangiaji mzuri katika medani za habari kwa kuwa na safu katika gazeti hilo hilo la serikali.

Mwanahabari Alfred Ngotezi