*Wadai akiwapuuza atakiona cha moto
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete asiunde Tume ya kusimamia mchakato wa Katiba mpya hadi hapo marekebisho waliyokubaliana yatakapo ingizwa kama walivyokubaliana.
CHADEMA kimesema kimeshangazwa na kusikitishwa kwa hatua ya Rais Kikwete kupuuza ushauri wao walioutoa hivi karibuni wakizungumza Ikulu wa kumtaka asitie saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 kabla ya wananchi kupewa fursa ya kutoa maoni na kuufanyia marekebisho.
CHADEMA wametoa kauli hiyo jana kupitia kwa Kaimu Katibu wake, John Mnyika, alipozungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam akitoa ufafanuzi juu ya kilichotokea tangu mazungumzo yao na Rais Ikulu.
Amesema wamemtaka Kikwete kutoendelea kuitekeleza kwa kuunda vyombo vya kusimamia mchakato huo kama Tume ya Katiba, kwani kufanya hivyo ni kintume na walichokubaliana katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu hivi karibuni.
Kusainiwa kwa muswada huo na Rais Kikwete, inamaana sheria hiyo inapaswa kuanza kutumika kuanzia Desemba Mosi, 2011.
Aidha Mnyika amemshauri Rais Kikwete na serikali yake kuahirisha kuanza kutumika kwa sheria hiyo na badala yake waanzishe utaratibu wa kuipeleka kwa wananchi ili ijadiliwe na kuitolea maoni, yatakayowasilishwa kwenye kikao kijacho cha Bunge kuifanyia mrekebisho.
“Tumeshangazwa na kusikitishwa na alichokifanya Rais, baada ya kukubaliana kwamba ipo haja ya muswada huu kufanyiwa marekebisho makubwa, sisi tulimshauri ni vema asisaini muswada huo kabla ya marekebisho kufanyika. Hatua ya Rais kusaini muswada huo itafanya kuwe na njia ndefu ya kurekebisha sheria hiyo…
“…tunajua Rais ameamua kusaini muswada huo bila kuzingatia ushauri wetu kwa sababu katiba mbovu ya sasa imempa mamlaka ya kusaini muswada wowote kuwa sheria bila kulazimika kusikiliza ushauri wa mtu yeyote.
Mnyika alisema lengo la CHADEMA ni kuona sheria hiyo inafanyiwa marekebisho makubwa katika kikao cha Bunge kitakachoanza Januari 31, mwakani. Ameongeza kuwa ikiwa sheria hiyo itaanza kutumika kama ilivyojieleza, basi nchi inaweza kuingia kwenye mgogoro na machafuko ya kisiasa kwani ina vifungu vingi vinavyokandamiza uhuru wa wananchi.
“…Moja ya vifungu vibaya kabisa vilivyomo kwenye sheria hiyo iliyosainiwa ni kifungu cha 19 ambacho kinakataza mtu au taasisi yoyote kukusanya maoni au kufanya shughuli ya kuwaelimisha wananchi kuhusu mabadiliko ya katiba. Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu atakayekiuka kifungu hicho atakuwa ametenda kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu hadi saba jela, au kulipa faini ya sh. milioni 5 hadi milioni 15, au adhabu zote kwa pamoja.
Amesema kifungu hicho na vingine vingi katika sheria hiyo, havikustahili hata kidogo kupitishwa na Bunge, kwani kinakiuka Katiba ya sasa ambayo imetoa uhuru wa maoni na haki ya wananchi kuelimishwa.
Hata hivyo Mnyika amesema CHADEMA inakamilisha maandalizi ya kuwatuma viongozi na makada wake nchi nzima kuanza ziara ya kufanya mikutano ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu ubovu na ubaya wa sheria iliyosainiwa na Rais ili waweze kuikataa na kutoa maoni yao.
Pamoja na hayo wametoa wito kwa wanaharakati, vyombo vya habari, viongozi wa dini na vikundi vyote vya kjamii kuungana katika kumshauri Rais na kushinikiza sheria hiyo isianze kutumika sasa.