Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Marekani, Barack Obama ametuma salamu za pongezi na kuitakia Tanzania maadhimisho mema ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tanzania Bara inatimiza miaka 50 ya Uhuru, Desemba 9, 2011.
Aidha, Rais Obama ameihakikishia Tanzania kuwa Marekani itaendelea kubakia rafiki na mshirika wa kuaminika katika jitihada za kuhakikisha kuwa Watanzania kujiletea maisha bora na kwa njia za amani.
Katika salamu zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais huyo wa Marekani ametumia lugha ya Kiswahili kuitakia baraka Tanzania akimwandikia Mheshimiwa Kikwete, “Mungu awabariki” na kufuatiwa na tafsiri ya maneno hayo hayo katika lugha ya Kiingereza.
Katika salamu zake, Rais Obama ameongeza kuwa umbali mkubwa wa kijiografia kati ya Tanzania unazidi kupungua kwa sababu ya uhusiano wa karibu kati ya Wamarekani na Watanzania.
Amesisitiza Rais Obama, “Hali ya kuwa anuwai ya taifa lako, kama ilivyo ya kwetu, ni chimbuko na msingi wa nguvu zitakazoipitisha Tanzania katika mabadiliko mengi na changamoto nyingi zinazokabili nchi yenye demokrasia inayopanuka.”