CUF nao waomba mazungumzo na Rais

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Ibrahim Lipumba

*JK akubali maandalizi yafanywa

Na Mwandishi Wetu

OFISI ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa taariza zaidi juu ya maombi ya CUF, iliyotolewa leo na Ikulu ni kwamba Rais Kikwete amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza wasaidizi wake kufanya maandalizi ya mkutano huo ili ufanyike mara moja.

CUF wanaomba kukutana na Rais Kikwete ikiwa ni siku chache baada ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuomba kukutana na Rais na kufanya mazungumzo kuhusiana na uundaji wa sheria inayoandaa mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania.

Hata hivyo mbali na taarifa ya Ikulu kutoa taarifa za ombi la CUF haikutaja ni mazungumzo ya kuhusiana na suala gani, ambayo Rais atafanya na chama hicho cha siasa ambacho kimeunda Serikali ya Mseto na CCM Zanzibar.