SHUGHULI za kuhesabu kura zinaendelea katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya uchaguzi mkuu hapo jana uliokumbwa na mashambulio ya waasi na machafuko katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Aidha watu waliokuwa wamejihami walishambulia kituo cha kupigia kura katika eneo la Lubumbashi na kuwauwa maafisa wawili wa Polisi na mwanamke mmoja. Pia walichoma magari manane yaliyokuwa yakisafirisha vifaa vya kupigia kura katika eneo hilo hilo.
Katika eneo la Kananga wapiga kura walichoma vituo vya kupigia kura na kuiba makaratasi ya kupigia kura baada ya kukasirishwa na kuchelewa kwa zoezi hilo.
Rais wa sasa Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu 2001 anakabiliana na wapinzani 10 wakiongozwa na mwanasiasa mkongwe, Etienne Tshikedi, huku zaidi ya wagombea elfu 18 wakiwania viti 500 vya ubunge. Matokeo rasmi ya urais yanatarajiwa tarehe 6 mwezi ujao, huku ya ubunge yakitarajiwa tarehe 13 mwezi Januari.
-DW