RAIA wasiopungua 23 wameuwawa nchini Syria huku jumuiya ya nchi za kiarabu ikiiwekea vikwazo nchi hiyo. Uingereza imeipongeza hatua hiyo ikisema ni ishara kushindwa kwa utawala kutimiza ahadi zake hakutapuuzwa.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria, limesema raia saba waliuwawa na maafisa wa usalama katika mkoa wa kati wa Homs, akiwemo mmoja aliyepigwa risasi alipokuwa katika paa la jengo moja katika mji wa Qusayr. Katika mji wa kaskazini wa Hama, watu watatu, akiwemo kijana wa miaka 17 waliuwawa kwa risasi wakati vikosi vya usalama vilipouvamia mji wa Karnaz.
Karibu na mji mkuu Damascus, watu 10 waliuwawa, akiwemo kijana wa miaka 14, huku wengine 13 wakajeruhiwa wakati maafisa walipofyetua risasi kiholela na kuwatia mbaroni watu kwenye uvamizi dhidi ya kitongoji cha Rankuss.
Machafuko hayo yalitokea wakati jumuiya ya kiarabu ilipouwekea jana utawala wa rais Bashar al Assad mfululizo wa vikwazo vya kidiplomasia na kiuchumi kwa kupuuza muda wa mwisho uliotolewa na jumuiya hiyo kwa Syria kuruhusu waangalizi wa kigeni kwenda nchini humo.
Mawaziri wa kigeni wa jumuiya hiyo walipiga kura kuunga mkono vikwazo vinavyojumuisha marufuku kwa maafisa wa utawala wa Syria kusafiri katika nchi wanachama, kuzuiliwa kwa akaunti za benki za serikali, marufuku ya biashara na serikali na kusitishwa kwa safari za ndege za nchi za kiarabu kwenda na kutoka Syria.
Joseph Kechichian, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, amesema, “Nchi zinazobakia upande wa Syria kwa sasa ni Iran na Lebanon. Ulimwengu mzima umeigeukia Syria na kuiwekea vikwazo. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa sana kwamba vikwazo hivi vitakuwa na athari.”
Irak na Lebanon hazikushiriki katika kuvipigia kura vikwazo vyote. Irak imetaja sababu za ushirikiano wa kibiashara na Syria, na huku ikiwa na wakimbizi wapatao milioni moja nchini humo, inahofia wanamgambo wenye siasa kali maadui wa Irak iwapo Assad ataangushwa madarakani. Lebanon pia haikuvipigia kura vikwazo hivyo kwa kuwa inaongozwa na kundi la Hezbollah, linalotambuliwa kuwa la kigaidi na mataifa ya magahribi, na ambalo ni mshirika wa karibu wa utawala wa rais Assad.Bildunterschrift:
Wakati huo huo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, William Hague, ameipongeza hatua ya jumuiya ya nchi za kiarabu kumuwekea vikwazo rais wa Syria, Bashar al Assad na kuutaka Umoja wa Mataifa uunge mkono uamuzi wa jumuiya hiyo. Hague aidha aliahidi kuisaidia jumuiya ya nchi za kiarabu katika jitihada za kurejesha amani ndani ya Syria na kuuonya Umoja wa Mataifa kwamba hauwezi kunyamaa kimya kuhusu ukandamizaji na mateso yanayoendelea nchini humo.
-DW