CHADEMA wakubaliana na Serikali, JK amaliza yaishe

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete (mwenye suti nyeusi) akiagana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe baada ya mazungumzo na mkutano na Rais Kikwete Ikulu.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hatimaye kimemaliza mvutano wake kati yake na Serikali ya CCM baada ya Rais Jakaya Kikwete kukubaliana na chama hicho katika vipengele kadhaa juu ya Sheria iliyopitishwa na Bunge kuandaa utaratibu wa kuelekea kuundwa kwa Katiba Mpya ya nchi.

CHADEMA ambayo wajumbe wake kadhaa wamefanya mazungumzo na Rais Kikwete kwa siku mbili mfululizo, jana wamefikia muafaka baada ya Serikali kukubali kufanyika kwa maboresho katika Sheria ya kuundwa tume inayoandaa mchakato wa Katiba mpya.

Kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na pande zote za mazungumzo, Serikali imekubali kuwa pamoja na Sheria hiyo kupitishwa na Bunge hivi karibuni ipo haja ya kuendelea kuboreshwa ili kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa.

taarifa hiyo pia imeeleza kuwa mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara yataendelea kati ya Serikali na wadau anuai juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha muafaka kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Katika mkutano huo kati ya viongozi waandamizi wa CHADEMA na Rais Kikwete, chama hicho kiliwasilishwa mapendekezo kabla ya Serikali kuyapitia na hatimaye kukubali yafanyiwe kazi ikiwa ni pamoja na kuiboresha sheria iliyokuwa ikisubiri saini ya Kikwete.

Chama hicho kikiungwa mkono na chama cha NCCR-Mageuzi wabunge wake waligoma kujadili muswada wa uundwaji wa sheria itakayosimamia na kujenga utaratibu wa kuundwa kwa tume itakayo kuwa na kazi ya kusimamia mchakato mzima wa kuundwa kwa Katiba Mpya.

Licha ya wabunge hao kutoka nje muda wote katika bunge lililomalizika hivi karibuni, lilipokuwa likijadili muswaada huo huku wakitaka uwasilishwe kwa mara ya kwanza na si mara ya pili kama ilivyofanywa. Kiburi chao kimezaa matunda baada ya Serikali kupokea hoja hizo na kuahidi maboresho katika sekta hiyo.