Dk. Shein amuapisha Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein leo mjini hapa amemuapisha Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma, Zanzibar katika hafla iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Hafla ya kuapishwa kwa Katibu huyo, Mtoro Almas wa Zanzibar ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Oisi ya Rais Fedham Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheri.

Viongozi wengine waliohudhuria kuapishwa kwa Katibu huyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib pamoja na viongozi wengine wa serikali.

Kabla ya Uteuzi huo Mtoro Almas aliwahi kuwa Meneja wa Mkuu wa Kiwanda cha Soda Zanzibar, Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Zanzibar, pia aliwahi kuwa Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar kilichopo Tunguu.

Uteuzi wa kiongozi huyo ulianza rasmi Novemba 20, Mwaka huu ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Shein alifanya uteuzi wa Katibu huyo wa Kamisheni ya Umma, Zanzibar kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu 22 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Zanzibar, No. 2 ya mwaka 2011.