Ni zaidi ya miezi mitatu tangu Sudan Kusini ilipojitenga na Sudan na kupata uhuru wake mwezi Julai mwaka huu. Kama nchi mpya Sudan Kusini imekuwa ikianzisha taasisi mbali mbali za kitaifa kama vile benki kuu, mahakama, bunge na fedha zitakazo tumiwa katika nchi hii mpya.
Lakini hata kwa kuzindua tasisi hizo, Sudan Kusini bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo kutotambuliwa kwa fedha zake na nchi jirani.
Ilhali ni jambo la kawaida kuweza kubadilisha fedha za nchi yeyote katika benki mbali mbali haswa katika nchi jirani, ni vigumu sana kubadilisha fedha za Sudan Kusini nchini Uganda au Kenya na hasa nchini Ethiopia.
Katika Jimbo la Upper Nile linalopakana na Jamhuri ya Sudan na Ethiopia, wafanyabiasha na wawekezaji kutoka Ethiopia, waliohojiwa na BBC walilalamika kwamba kukataliwa kwa pauni za Sudan Kusini na benki kuu nchini Ethiopia kunaathiri biashara zao.
“Tukiuza bidhaa zetu, ni lazima tutafute jinsi ya kuenda Juba na kubadilisha hizi pauni na dola za Marekani ili tuweze kwenda nyumbani na kununua bidha zingine au kuona familia zetu. Mara nyingi kama msimu wa mvua, tunajikuta hatuwezi kuondoka kutoka Nasir kwa sababu hakuna barabara kwenda Juba na inabidi tutegemee mashua ambazo huchukua wiki mbili kufika au kumtuma mtu anayekwenda Juba akubadilishie fedha. Kwa ajili hiyo, tunapoteza fedha nyingi sana” alisema Mulu Jelet mchuuzi kutoka Ethiopia mjini Nasir, katika Jimbo la Upper nile.
Licha ya malalamiko ya wafayabiashara, meneja wa benki moja mjini Gambella nchini Ethiopia ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alithibitisha kwamba hawachukui fedha za Sudan Kusini kwa sababu hazikuwa na tarehe.
Nchini Kenya vile vile, fedha za Sudan Kusini pia hazikubaliwi katika maduka ya kubadilisha fedha, jambo ambalo linawatatiza wafanyabiashara na watu wanaojitafutia riziki katika nchi hii mpya. Ofisi moja ya kubadilisha pesa iliyo mjini Nairobi ilisema kwamba hawazichukui fedha za Sudan Kusini kwa sababu bado hawana uhakika na thamani yake.
Licha na hili, raia wa Afrika mashariki walio Sudan Kusini wanaendelea kuongezeka huku biashara kati ya nchi hizi ukiendelea kukita mizizi kwani nchi hii mpya inaagiza zaidi ya asilimia 70 ya vyakula vyote na bidhaa za matumizi kutoka nchni jirani na hasa Uganda na Kenya.
-BBC