Zimbabwe yainyoa Djibouti Kombe la Tusker


Mmoja wa wachezaji wa Djibouti akinyoosha mkono kuomba msaada kwa mwenzake aliyeanguka chini.

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Zimbabwe leo mchana imefanikiwa kiibanjua timu ya Djibouti mabao 2-0, katika Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Zimbabwe katika mchezo huo walionekana kuwakamia vijana wa Djibouti hivyo kuwashambulia muda wote katika lango lao tangu dakika za mwanzo za mchezo huo. Vijana wa Zimbabwe walianza kufungua kitabu cha magoli katika dakika ya tisa tu ya mchezo ambapo mchezaji wa hatari, Donald Ngoma aliandika bao la kwanza.

Mchezaji Ngoma wa Zimbabwe ndiye aliyekuwa mwiba kwa timu ya Djibouti kwani aliwachachafya muda wote mabeki wa timu pinzani. Karamu ya magoli kwa Wazimbabwe iliendelea tena ambapo katika dakika ya 73, mchezaji Qadr Amini aliipatia tena bao timu yake.

Hadi mwisho wa mchezo huo Zimbabwe iliibuka na magoli 2 huku, Djibouti, vijana wa Kisomali wakiondoka patupu. Mchezo unaofuata majira ya saa kumi ni Watanzania wa Zanzibar pamoja na Burundi ambao tayari wanapointi tatu za mechi yao ya kwanza.