Chadema ngangari

dr-slaa

  • Chasisitiza kuendeleza maandamano
  • Chasema ni uamuzi wa Kamati Kuu
  • Chasema si ya kuiangusha serikali

Na Khamis Mkotya
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesisitiza kuwa kitaendeleza maandamano ya amani nchi nzima.

Kimesema kitafanya hivyo licha ya viongozi wa Serikali kulalamikia maandamano ya chama hicho yaliyofanyika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni.

Uamuzi huo ni agizo la Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyokutana Dar es Salaam juzi kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa mipango ya chama hicho, hali ya siasa na taarifa ya maandamano ya kanda ya ziwa.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alikuwa akisoma maazimio ya kamati hiyo Dar es Salaam jana.

Alisema kamati kuu ilijadili kwa kina suala la maandamano na ujenzi wa chama na hivyo imeagiza kiendeleze maandamano.

Hata hivyo, Mbowe alisema kamati kuu ya chama chake imesikitishwa na kauli za baadhi ya viongozi wa Serikali wanaobeza maandamano hayo huku wakipotosha umma kwamba yanalenga kuchochea vurugu.

“Viongozi wa Serikali wanahofu ya kupoteza madaraka na nyadhifa walizonazo, sasa wanaigeuza hofu yao kuwa hofu ya taifa. Kimsingi wananchi hawana hofu yoyote juu ya maandamano ya chama chetu, bali wao ndiyo wenye hofu na nyadhifa zao,’’ alisema.

Mbowe alisema maandamano ya chama chake hayana lengo la kuiangusha Serikali kama inavyotafsriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, bali yanalenga kuwashukuru wananchi kwa imani yao kwa chama hicho.

“Katika mikutano yetu ya Kanda ya Ziwa hatujawahi hata siku moja kuwaambia wananchi wakaiondoe kwa nguvu Serikali halali iliyopo madarakani. CHADEMA ni chama makini, kitaendelea kutafuta ridhaa ya wananchi ya kuunda Serikali kwa njia za kidemokrasia,” alisisitiza.

Mbali ya mawaziri kulalamikia maandamano hayo hata Rais Jakaya Kikwete naye aliishutumu CHADEMA kwamba kinakusudia kuiangusha serikaki kwa nguvu.

Chama cha CUF pia kimekuwa kikionya juu ya maandamano hayo ya CUF kikisema yana lengo la kuiondoa serikali katika madaraka, jambo ambalo ni uhaini.

Mbowe alidai wasiwasi na hofu aliyonayo Rais Kikwete inatokana na kile alichokiita kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alisema baada ya maandamano ya kanda ya ziwa yaliyofanyika kwa mafanikio makubwa, sasa chama chake kinaelekeza nguvu ya maandamano Kanda ya Nyanda za Juu za Kusini yatakayoanza Mei 4, mwaka huu yakihusisha mikoa ya Iringa, Mbeya na Ruvuma na baadaye Morogoro.

Alisema maandamano hayo pamoja na kuwashukuru wananchi lakini pia yanalenga kuendelea kuibana Serikali kuchukua hatua za kupunguza adha ya gharama za maisha.

Chama hicho pia kimetangaza kusudio la kumfikisha mahakamani Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba iwapo atashindwa kuthibitisha madai yake kwamba maandamano ya chama hicho yanafadhiliwa na nchi za nje.

Mbowe alisema kauli ya Simba imelenga kuchafua uhusiano wa chama hicho na jumuiya za kimataifa.

Alisema maandamano ya kanda ya ziwa yamefanyika kutokana na michango ya wananchi ambako wabunge wa chama hicho walichanga Sh milioni 19 kufanikisha maandamano hayo.

Kuhusu mgogoro wa siasa wa Arusha, chama hicho kimepinga ushauri wa Serikali wa kukitaka kwenda mahakamani kupinga uchaguzi wa umeya wa Arusha kikisema kuwa uchaguzi uliofanyika haukufuata taratibu na sheria za uchaguzi.

Kwa sababu hiyo, chama hicho kimeipa Serikali siku 21 kumaliza mgogoro huo kwa kuitisha upya uchaguzi wa meya vinginevyo nguvu ya umma itatumika kuhakikisha uchaguzi wa halali unarejewa.

“Kwa kuzingatia Serikali imeziba masikio kusikia busara zilizotolewa juu ya namna ya kutatua mgogoro wa umeya wa Arusha, Kamati Kuu kwa mara ya mwisho inaitaka Serikali kumaliza mgogoro wa umeya ndani ya siku 21.

“Baada ya muda huo, CHADEMA haitakuwa na uwezo tena wa kuwazuia wananchi wa Arusha kudai uchaguzi wa meya wao kwa njia ya nguvu ya umma,” alisema Mbowe na kuongeza.

“Hoja hapa si CHADEMA kushinda, hoja ni kufanyika kwa uchaguzi wenye kufuata taratibu na sheria. Hatuna tatizo na CCM kushinda umeya, hata ashinde wa TLP kama taratibu zimefuatwa tutampongeza na tutampa ushirikiano. Meya wa sasa ametokana na hila,” alisema Mbowe.

Kuhusu tatizo la umeme nchini, chama hicho kimeitaka Serikali kupitia upya mikataba ya umeme kwa vile tatizo la umeme linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikataba hiyo ambayo kimesema mingi imetokana na rushwa.

Mbowe alisema tangu Serikali ilipoingia mkataba na kampuni ya IPTL mwaka 1991, haijawahi kuwa na mkakati wa kuwa na umeme wa uhakika.

CHADEMA imeitaka Serikali kuachana na utaratibu wa kukodisha mitambo ya umeme na badala yeke inunua mitambo yake kumaliza tatizo hilo.

“Hakuna waziri asiyekuwa na jenereta nyumbani kwake, kuanzia maofisini hadi majumbani mwao wanatumia majenereta ambayo gharama za ununuzi pamoja na mafuta yanayotumika ni fedha za umma. Hawa watu hawajui machungu ya mgao wa umeme,” alisema.

Kuhusu deni la taifa, chama hicho kimeshangazwa na kupanda kwa kasi kwa deni hilo hadi kufikia dola za Marekani milioni 11 ambalo ni ongezeko la asilimia 18 kwa mwaka.

Chama hicho kimemtaka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kutoa maelezo ya kina kuhusu kupanda kwa deni la taifa.

Chanzo:gazeti la Mtanzania