Mawaziri tisa wa Kikwete ni hatari`

 

Mh. Zitto Kabwe

 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, amesema mawaziri tisa wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wanatishia uchumi wa nchi kutokana na kuendekeza vita vya kuusaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa mwaka 2015.

Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), japo hakuwataja mawaziri hao, alitoa madai hayo muda mfupi mara baada ya kufungua mkutano wa Muungano wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA) jijini Dar es Salaam jana.

Mkutano huo uliojumuisha vijana kutoka katika nchi 22, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) ndio wenyeji wao hapa nchini.

“Mawaziri tisa, tunao nchini, wanaacha kufanya kazi wanaingia katika ugomvi. Mbona bado miaka minne Rais Kikwete ametoa ahadi kibao zitatekelezeka vipi ikiwa viongozi wenyewe ndio wapo katika ugomvi na wanashindwa kusimamia maendeleo ya nchi na kuiweka nchi katika sehemu nzuri kiuchumi?” alihoji Zitto.

Zitto, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Uchumi, hakuwataja mawaziri hao.

Alisema anashangaa kuona Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokaa Dodoma hivi karibuni, kushindwa kutoa maamuzi mazito, badala yake inatoa maamuzi ya ajabu.

Zitto alisema alifikiri maamuzi ambayo yangetolewa na CC, ni ya kuwatimua mawaziri walioingia katika ugomvi wa urais na kuteuliwa wengine ambao wanaweza kufanya kazi.

Alisema kinachotakiwa kwa sasa kama Rais Kikwete amebakiwa na nafasi saba za viti maalum, basi awatimue mawaziri wanaotaka urais kwa sasa na awateue wengine, ambao watafanya kazi kwa ufasaha na kuinua nchi kimaendeleo.

Zitto alisema hivi sasa uchumi wa Tanzania umeporomoka kufikia asilimia 17.

Alisema hali hiyo imesababishwa na mawaziri hao kushindwa kufanya kazi za kujenga uchumi wa nchi, badala yake kujiingiza katika vita hivyo.

Zitto, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kwa sasa hali ya nchi ni mbaya ukilinganisha na wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, ambao alisema uchumi ulishuka kwa asilimia 4.5.

Hata hivyo, alisema anamshukuru Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, kwa kukiri kuchafuka kwa hali ya hewa ndani ya chama hicho kwamba, kunatokana na mbio za urais wa mwaka 2015.

Alisema Mukama alisema kuchafuka kwa hali hiyo ndani ya kumesababisha kuwako kwa makundi makubwa mawili yanayopingana.

Zitto alisema kutokana na kauli hiyo, CCM imepoteza nguvu, huku mawaziri wake hao kila mmoja macho yake yapo katika urais kiasi cha kuingia katika ugomvi na kuacha kufanya kazi za kuimarisha uchumi wa nchi unaoyumba kwa kiasi cha kutisha.

Alisema kama mawaziri wameingia katika ugomvi wa kutaka nafasi ya urais, ni dhahiri kwamba, hakuna waziri atakayesimamia maendeleo ya nchi hasa kwenye madini, umeme na kudhibiti tatizo la kushuka kwa shilingi.

Zitto alisema hali hiyo ni hatari hasa kwa taifa linaloendelea.

Kuhusu kauli ya CCM kutaka vyama vingine viungane na Chadema katika kumuona rais, Zitto alisema chama chake kimeshatoa tamko na kama kuna chama kinahitaji kufanya hivyo, basi kiombe siku zao nyingine na wafanye mazungumzo yao.

“Hapa CCM inadandia hoja yetu. Kama kuna vyama, ambavyo vinataka kukutana na rais, basi wapange siku yao waweze kukutana nao waweze kuzungumza yao na si kudandia katika chama chetu,” alisema Zitto.

Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, alisema katika mkutano huo mada kuu ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati ya vyama vyao kutumia kampeni za kisayansi ili kushinda chaguzi mbalimbali.

Alisema mambo mengine wanayojadili, ni pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali za Afrika zinatumika kwa kuwanufaisha Waafrika wenyewe na jinsi ya kupiga vita rushwa na uzembe .

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI