Na Joachim Mushi
KILA ifikapo Novemba 19 mataifa mbalimbali ulimwenguni hufanya maadhimisho ya siku ya choo duniani. Kimsingi tunafanya maadhimisho ya siku hii ili kutambua umuhimu wa choo, kuwa na choo safi.
Tanzania bado idadi kubwa ya familia hazina vyoo na hazitumii vyoo katika haja zake. Mfano kwa Jiji kama Dar es Salaam zaidi ya mabasi ya abiria 100 yenye idadi ya abiria 65,000 yanaingia na kutoka katika mji huu kila siku.
Mizunguko hii ya abiria kwa siku moja ambao hutumia takribani siku nzima au nusu siku barabarani hujisaidia hovyo barabarani. Baadhi si kwamba wanapenda bali wanafanya hivyo kutokana na Serikali kutokuwa na vyoo vya umma vinavyo wawezesha abiria hawa kutimiza haja zao wawapo safarini.
Kwa mantiki hiyo zaidi ya watu 6,500,000 (abiria tu) kwa siku hawatumii vyoo hivyo kujisaidia hovyo barabarani. dev.kisakuzi.com imefanya utafiti mdogo hivi karibuni mikoa ya kusini na kushuhudia hali hii katika picha. Tazama picha mbalimbali ambazo mtandao huu umezinasa.
Hata hivyo taasisi ya WaterAid hivi karibuni imetoa semina kwa wanahabari kuhusiana na umuhimu wa matumizi ya vyoo kwa familia mbalimbali nchini pamoja na usafi kiujumla. Semina ambayo ilifanyika siku moja kabla ya kuadhimisha siku ya choo duniani.
WaterAid inaamini elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo na usafi, ikiwa ni pamoja na taasisi anuai ikiwemo Serikali kutimiza wajibu wake yanaweza kufanyika mapinduzi tofauti na ilivyo sasa.
Kwa Tanzania takwimu zinabainisha kuwa takribani watoto 20,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ufariki dunia kutokana na magonjwa ya kuharisha, ambayo husababishwa na uchafu ikiwemo utelekezaji vinyesi.