Chama Cha Mapinduzi njia panda

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara akionekana mwenye kufikiri jambo.

Chadaiwa kilikurupuka kujivua gamba, sasa kimekwama

WAKATI CCM imemaliza vikao vyake vikuu vya maamuzi mjini Dodoma juzi bila kufikia kikomo cha dhana yake ya kujivua gamba, wasomi, wanaharakati nchini wamedai chama hicho tawala kilikurupuka ndiyo maana imeshindwa kutekelezeka.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, wasomi, wanaharakati na wanasiasa hao walisema kuwa, chama hicho hakikufanya utafiti wa kina kujua madhara ya mkakati wake wa kujivua gamba kabla ya kuutangaza, matokeo kimeshindwa kufikia mwafaka na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wameuacha kiporo kwa Kamati Kuu ya chama hicho.

Walisema kuwa, kama chombo kikubwa cha maamuzi cha chama (NEC) kimeshindwa kulimaliza jambo hilo na kulirudisha kwenye vikao vya chini badala ya kulipelekea kwenye kikao cha juu (Mkutano Mkuu) maana yake uhusiano wa chama na wanachama wake umekufa na kuna mgogoro mkubwa wa kidemokrasia ndani ya chama.

Kauli za wasomi
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM), Bashiru Ally alisema suala la kujivua gamba limetoa picha mbili ndani ya CCM.

Mosi, Dk Ally alisema inawezekana jambo hilo limerudishwa kwenye Kamati Kuu ili lipotee ‘kiaina’ kwa madai ya kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani watuhumiwa wa ufisadi wanaodaiwa kukipunguzia umaarufu chama hicho miongoni mwa umma.

Picha ya pili alisema ni kufa kwa uhusiano wa chama na wanachama wake, kwa sababu chombo kikubwa cha maamuzi kama NEC kinaposhindwa kuamua, ni dhahiri kuna tatizo kubwa ndani ya chama.

“Kama kujivua gamba ni mageuzi makubwa, basi yangepelekwa kwa wanachama halafu hatua zingeendelea hadi kufikia Mkutano Mkuu. Kama hili halifanyiki basi kuna mgogoro wa demokrasia ndani ya chama,” alisema Bashiru.

Aliongeza kuwa tatizo lingine ndani ya CCM ni kufa kwa utamaduni wa mijadala na kwamba, matatizo ndani ya chama hayawezi kumalizwa ndani ya vikao viwili pekee.

Bashiru alibainisha kuwa kilichotokea juzi Dodoma ilikuwa ni shughuli za makundi, lakini utendaji wa chama kwa upana na marefu yake.

Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma wa UDSM, Dk Benson Bana aliweka wazi kwamba, kujivua gamba haukuwa mkakati wala kauli mbiu stahiki kwa chama hicho.

Dk Bana alifafanua kuwa dhana hiyo, haikuchambua maana halisi ya gamba lenyewe, ndio maana utekelezaji wake umekwama.

“Mimi naona kujivua gamba kama kauli mbiu ambayo haikustahili, kwa vile maana yake ni pana sana. Magamba ni yapi au ni nani? Jambo hili walishindwa kuliweka bayana tangu awali na sasa linawashinda,” alisema Dk Bana.

Alieleza kuwa kujivua gamba kuliwahusu watu wachache ndani ya chama na sasa watu hao wamejisafisha na badala ya kuwa magamba, wanaonekana kupata nguvu zaidi ndani na nje ya chama hicho.

“Zile zilikuwa tuhuma tu, hatuwezi kumhukumu mtu kwa kumtuhumu,” alisema Dk Bana.

Aliishauri CCM kujiimarisha kwenye ngazi ya matawi na kubadilisha mkakati wa kujivua gamba haraka kwa kuwa hauna tija kwa chama hicho.

Mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma wa UDSM, Dk Bakari Mohamed, alisema dhana ya kujivua gamba haikupaswa kuwalenga baadhi ya watu, bali ilipaswa kuangalia mfumo mzima wa chama kuanzia ngazi ya matawi hadi taifa.

Alisema anaamini kuwa wakati CCM inakuja na mkakati huo hawakujua tatizo lilikuwa wapi na pengine hata dhana hiyo imekuja kwa shinikizo tu bila maono ya mbali.

“Ni suala gumu, watawafukuza wangapi? Ndio maana wameona mchezo huu utawapeleka pabaya,” alisema Dk Mohamed.

Wanaharakati
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananelia Nkya, alisema dhana ya kujivua gamba, imekosa mwelekeo kwa kuwa haikupata tafsiri sahihi tangu awali.

“Dhana haikuwa haikufafanuliwa mapema kuwa nani ana gamba na nani hana, Mwanzo haukuwa mzuri ni kama walikurupuka,” alisema Nkya na kuongeza;

“Kama ni kusafisha chama, wangeweka wazi uchafu ni huu na ule, ili watu wajue wana gamba au hawana. Lazima wakae kama chama wafafanue gamba ni nini”

Kwa mujibu wa Nkya, bila mambo hayo kufanyika, CCM kitaendelea kuwa chama kifisadi na mwisho wake hautakuwa mzuri.

Kauli za wanasiasa
Kwa upande wake Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid, alisema kinachowasumbua CCM ni kushindwa kufanya maamuzi magumu.

Rashindi alifafanua kuwa kitendo cha agenda kufikishwa ngazi za juu kwa ajili ya kutolewa maamuzi na kurudishwa tena ngazi za chini, huko ni kutetereka kwa chama.

“Jambo kama hilo la mageuzi ni kubwa. Kama mmefikia hatua ya kufanya maamuzi ni busara yafanyike haraka, kuchelewa ni kuendeleza matatizo ndani ya chama na yatahamia hata katika utendaji wa serikali,” alionya mwanasiasa huyo ambaye pia aliwahi kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni

Nape Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye alipozungumza na gazeti hili kuhusu utata wa dhana ya kujivua gamba alisema: “Suala hili lilikuwa na pande mbili ambazo zote zilipitia hatua stahiki. Upande wa kwanza ulikuwa ni kwa watuhumiwa kujipima wenyewe na kuchukua hatua au chama kiwachukulie hatua.”

Aliongeza kuwa baada ya miezi saba kupita, wamewasilisha taarifa yao NEC kwamba , upande wa kwanza wa watuhumiwa kujipima na kuchukua hatua, haujatekelezwa.

“Tumewasilisha ripoti yetu kuwa mwitikio wa kujipima haukuwa mkubwa mbali na yule mmoja aliyejiuzulu na Halmashauri Kuu imetuambia tukatekeleze awamu ya pili ambayo ni chama kuwachukulia hatua,” alisema Nape.

Naye Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Chadema, John Mnyika, alisema sakata hilo linaonyesha wazi kuwa NEC ya CCM haina uwezo wa kuchukua hatua.

Mnyika alifafanua kuwa mtu anapotuhumiwa, kwanza anapaswa kuandikiwa barua ya kuelezwa makosa yake ili ajitetee, kisha kuhukumiwa.

“Tangu Aprili hawajafanya hivyo suala hili limerudi kwenye Kamati Kuu kwa sababu halikuchukuliwa hatua mapema,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo.

Mnyika aliendelea kueleza kuwa CCM inachofanya ni sawa na kuwatapeli wananchi kwani waliwakumbatia mafisadi tangu mwanzo na sasa wanadai kuwa wanataka kupambana nao.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema suala la kujivua gamba ni danganya toto ya CCM, lakini mwisho wa mchezo huo ni upatikanaji wa Katiba mpya.

Katika kikao chake cha Aprili mwaka huu, Halmashauri Kuu ya CCM ilitangaza mkakati wa kujivua gamba kwa kuwaagiza wanachama wake wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi wawajibike.

Mkakati huo ulioridhiwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete, ulilenga kukisafisha chama hicho, kukipa sura mpya, hata hivyo haujatekelezwa hadi sasa kwani kinyume na matarajio ya wengi kuwa NEC iliyomalizika wiki iliyopita Dodoma ingetumia panga lake kuengua makada wanaoandamwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, suala hilo limerudishwa Kamati Kuu, kwa hatua zaidi.

Hadi sasa ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz peke yake aliyetangaza kujivua gamba kwa kuachia kiti hicho na nyadhifa zingine zote ndani ya chama hicho, miongoni mwa viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kwa masuala mbalimbali ya ufisadi.
CHANZO: Mwananchi