Na Hilda Mhagama
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal amewataka Watanzania kuitumia fursa ya elimu huria inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwani ni elimu bora ya juu inayotolewa kwa njia ya masafa.
Dk. Bilal ametoa changamoto hiyo leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mahafali ya 23 ya Chuo hicho yaliyofanyika kwenye eneo la Bungo, Kibaha mkoani Pwani sehemu ambayo chuo hicho kinajenga makao yake makuu.
Aidha ameongeza kuwa kujengwa kwa Makao Makuu ya OUT Kibaha ni fursa mpya na muhimu kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani, kwani idadi ya vyuo vya Elimu ya Juu katika Mkoa wao ni ndogo ikilinganishwa na Mikoa mingine.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ya juu alisema kubwa ni uhaba wa wahadhiri wenye sifa ili kwendana na mahitaji na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na vyuo, hasa kwa chuo hicho ambacho kwa sasa kina idadi kubwa ya wanafunzi.
Hata hivyo ameshauri OUT kushirikiana na vyuo vingine nchini katika ukuzaji wa mfumo wa elimu ya masafa jambo ambalo amesema linaweza kukikwamua kwa baadhi ya changamoto.
Pamoja na hayo Dk. Bilal ametoa pongezi kwa viongozi na maofisa waandamizi wa Serikali wakiwemo mawaziri, mabalozi, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wajasiriamali kutoka nyanja zote waliofanikiwa kutunukiwa shahada na stashahada chuoni hapo.