Na Joachim Mushi
PROFESA wa Chuo Kikuu cha Elimu UDSM, Herme Mosha amesema Tanzania haiwezi kujivunia kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru ikiwa hadi leo asilimia 50 ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi wanafeli na huku asilimia 80 ya walimu wa shule za msingi ni waliopata daraja la tatu kushuka chini.
Profesa huyo mkongwe kutoka tasnia ya elimu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la kujadili Hali ya Elimu Katika Miaka 50 ya Uhuru nchini lililoandaliwa na Umoja wa Wanafunzi wa Ualimu UDSM kwa kushirikiana na taasisi ya Hakielimu.
Alisema wakati Tanzaia ikijipanga kusherehekea miaka 50 ya Uhuru bado kuna dosari nyingi katika sekta hiyo jamboa ambalo anasema juhudi zikifanywa yanaweza kufanyika mabadiliko makubwa.
Alisema asilimia 10 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kile cha tano wanapata daraja la II na III, huku hadi leo bado kuna sehemu wanafunzi hasa shule za msingi wanasoma wakiwa wamekaa chini.
“Kimsingi bado tupo nyuma sana ukilinganisha na elimu ambayo ilikuwa ikitolewa nchini miaka ya 1961 hadi 1967, kupitia sera mbalimbali zilizokuwa zikitekelezwa. Mwanafunzi aliyesoma enzi zile alikuwa ameandaliwa vizuri ukilinganisha na wasasa…hii ni kwasababu tulikuwa tunafanya vizuri maeneo yote kuanzia walimu, vifaa, madarasa…,” alisema Prof. Mosha.
Alisema Tanzania ina sera nzuri za elimu lakini kikwazo kikubwa ni utekelezaji wa sera hizo. “Tanzania kisera hatuna tatizo bali tatizo lipo katika utekelezaji. Naamini kikwazo kipo katika bajeti..ukiangalia katika bajeti zetu kwenye sekta ya elimu hakuna kipindi ambacho bajeti inavuka asilimia mbili ya pato la taifa,” alisema.
Miongoni mwa wasomi wengine ambao walitoa mada ni pamoja na Dk. Hillary Dachi na Dk. Kitila Mkumbo. Kongamano hilo ambalo limeambatana na mijadala kwa wanafunzi wa ngazi zote, wadau wa elimu linatarajiwa kutoka na majumuisho ambayo yatapelekwa kwa wadau wa sekta husika.