Na Mwandishi Wetu
BINGWA wa Michuano ya Kombe la Uhai anatarajiwa kujulikana leo baada ya mechi ya fainali ya michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Kombe hilo (Uhai Cup) kwa klabu za Ligi Kuu kufanyika leo majira ya saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume.
Awali fainali hiyo kati ya Simba ambayo iliingia hatua hiyo kwa kuitandika Toto Africans mabao 4-1 na Azam iliyofuzu kwa kuizamisha Serengeti Boys (timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17) mabao 3-0 ilikuwa ichezwe leo (Novemba 25 mwaka huu) saa 9.00 kwenye uwanja huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi za michuano ya Kombe la Tusker Chalenji iliyoanza Novemba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.
Wambura alisema kwa kila siku kwenye michuano ya Tusker Chalenji zinachezwa mechi mbili; huku ya kwanza ikianza saa 8.00 mchana na ile ya pili ikipigwa majira ya saa 10.00 jioni.
Aidha ameongeza kuwa viingilio katika mechi hizo za hatua ya makundi kwa michuano ya Kombe la Tusker Chalenji iliyoanza Novemba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vitakuwa kama ifuatavyo;
“Kwa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni zaidi ya 30,000 kiingilio kitakuwa sh. 1,000 wakati viti vya rangi ya chungwa ambavyo ni zaidi ya 10,000 kiingilio kitakuwa sh. 3,000. VIP C na B ambayo jumla ya viti vyake ni 8,000 kiingilio kitakuwa sh. 5,000 wakati VIP A yenye viti 700 kiingilio ni sh. 10,000,” alisema Wambura.
Akifafanua zaidi kwenye michuano ya Kombe la Uhai, amebainisha kuwa inadhaminiwa na Kampuni ya S.S. Bakhresa kupitia maji Uhai ambapo bingwa atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba.
Mchezaji bora sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu sh. 300,000.