Mkwasa ataja kikosi cha michuano ya Kombe la Tusker Chalenji

Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa

KOCHA Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa ametaja kikosi cha mwisho cha wachezaji 20 kwa ajili ya michuano ya Tusker Chalenji inayoanza kesho.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema wachezaji waliobaki na timu zao kwenye mabano kati ya 28 waliokuwa wameitwa awali ni pamoja na Juma Kaseja (Simba), Shabani Kado (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga) na Juma Jabu (Simba).

Aidha aliwataja wengine ni Ibrahim Mwaipopo (Azam) na Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Nurdin Bakari (Yanga), Haruna Moshi (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Simba).

Wambura amesema wengine ni Said Maulid (Angola), Musa Mgosi (DC Motema Pembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC), Mrisho Ngassa (Azam), Ramadhan Chombo (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Rashid Yusuf (Coastal Union).
Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ya kwanza Novembe 26 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

Wakati huo huo Wambura amesema, timu ya Taifa ya Zimbabwe (Might Warriors) imeteuliwa na CECAFA kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza Novemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam kuziba nafasi ya Namibia iliyojitoa.

Zimbabwe itawasili Novemba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam na itakuwa kundi A pamoja na timu za Tanzania Bara, Rwanda na Djibouti.